Lugola awakaribisha wananchi wampe kero zao

Muktasari:

Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola kesho Jumamosi Agosti 10, 2019 anaanza ziara ya siku tano mkoani Rukwa ambapo amewaomba wananchi kujitokeza katika mikutano ya hadhara atakayoifanya kumpatia kero zao ili aweze kuzitatua.

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola amewataka wananchi mkoani Rukwa kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya hadhara atakayoifanya kwa lengo la kumpa kero zinazowakabili ili aweze kuzitafutia ufumbuzi.

Lugola amesema hayo leo Ijumaa Agosti 9, 2019 mkoani Iringa ambapo ametumia fursa hiyo kuwataka polisi mkoani humo kutenda haki katika utendaji wao.

Taarifa iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano cha wizara yake imesema Waziri Lugola amesema hayo baada ya kufanya ziara fupi mkoani Iringa akiwa safarini kwenda Mkoa wa Rukwa kwa ziara ya siku tano.

Akizungumza katika kikao cha viongozi wa Polisi Mkoa wa Iringa, Lugola amesema amefika kuonana na viongozi hao akiwa safarini kwa lengo la kufuatilia utendaji kazi ikiwa ni utaratibu wake ambao alijiwekea tangu aiongoze wizara hiyo.

Lugola amesema lengo la ziara yake mkoani Rukwa ni kufuatilia maagizo yake aliyoyatoa kwa vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo ndani ya wizara yake na pia atafanya ziara kama hizo mikoa yote nchini.

Amesema anatarajia kutembelea wilaya zote za Mkoa huo kusikiliza kero za wananchi kupitia mikutano mbalimbali ya hadhara itakayofanyika katika wilaya hizo.

“Natarajia kuanza ziara hiyo rasmi kesho Agosti 10, 2019  Mjini Sumbawanga kwa kukutana na mkuu wa mkoa pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, kupokea taarifa ya kamati hiyo.”

“Kabla ya kuanza kuzungumza na wakuu wa vyombo vyake na baadaye kukutana na Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa na kumaliza kwa kuzungumza na Baraza la Askari na Watumishi wote wa Wizara hiyo waliopo mjini humo,” amesema Lugola.

“Nitafanya mkutano mkubwa wa hadhara katika Mji wa Sumbawanga, utaanza saa 10:00 hadi 12:00 jioni, hivyo nawaomba wananchi wa mji huo wajitokeze kwa wingi kunisikiliza kile ambacho nimepanga kuwaambia na pia nitawapa nafasi wananchi waulize maswali bila woga, waniambie kero zao nami nitazitatua katika mkutano huo,” amesema Lugola. 

Lugola amesema katika ziara yake aliyoifanya mikoa ya Kigoma, Kagera, Arusha, Februari na Morogoro kwa nyakati tofauti amegundua wananchi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali hivyo hawezi kulala akiwa ofisini, lazima afanye ziara nchi nzima kuwasaidia wananchi kutatua kero zao ambapo wengi wao wakiwalalamikia polisi wakiwaonea.

“Kupitia kikao hiki hapa Iringa, napenda kuwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi, wanapojitokeza kwa wingi inasaidia kusikiliza matatizo yao yanayowakabili, ndio maana nimepanga kufanya ziara kama hizi nchi nzima.”

“Hii inasaidia sana kujua matatizo mbalimbali ya wananchi pamoja na kuangalia utendaji kazi wa taasisi zangu zilizopo ndani ya wizara hii,” amesema