VIDEO:Lugola awaondoa hofu Watanzania kuhusu tishio la ugaidi

Thursday June 20 2019

Kangi Lugola,Siku ya Wakimbizi Duniani,Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania,

 

By Tumaini Msowoya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Kangi Lugola amewatoa hofu Watanzania akiwataka wasiwe na hofu wala wasiwasi kuhusu tahadhari iliyotolewa na Ubalozi wa Marekani kuwa kuna fununu za mipango ya mashambulizi katika Jiji la Dar es Salaam.

Lugola ametoa tahadhari hilo leo Alhamisi Jun1 20, 2019 wakati akizungumza katika maadhimisho ya siku ya wakimbizi iliyoandaliwa na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR).

"Tahadhari iliyotolewa na wenzetu wa Ubalozi wa Marekani ni taarifa ya kawaida waliyoipata wenzetu na tumewasiliana, Watanzania wasiwe na hofu wala wasiwasi nchi yao ina amani," amesema Lugola

Amesema vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kufanya kazi vyombo viachwe vifanye hivyo.

"Ni tahadhari kama zile za sunami, mvua nyingi na nyingine mbalimbali, Serikali itahakikisha wananchi na mali za wananchi zinalindwa," amesema.

Awali, Mwakilishi wa UNHCR nchini Tanzania, Chansa Kapaya anasema siku ya wakimbizi inatoa nafasi ya kutafakari na kukumbuka kwamba wakimbizi ni watu na wanatamani nchi zao ziwe na amani waweze kurejea.

Advertisement

"Tunaunga mkono Serikali ya Tanzania katika kutoa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na chakula, mavazi, maji safi na makazi," amesema.

Mpaka Mei 2019 Tanzania ilikuwa inahifadhi wakimbizi 312,152 wengi wao walitokea Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Jana Jumatano Juni 19, 2019 Ubalozi huo ulieleza kuwapo kwa uvumi wa kutokea kwa shambulio la kigaidi katika eneo la Masaki hususan hoteli za kitalii na maduka ya maeneo hayo ya ufukwe wa Bahari ya Hindi.

Ubalozi huo uliwataka wakazi kuwa makini na maeneo hayo, kujiepusha na makundi na kufuatilia taarifa kupitia vyombo vya habari.

 


Advertisement