Lugola azungumzia shambulio la Lissu, amtaja dereva wake

Muktasari:

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ametilia shaka maelezo ya Adam Bakari, dereva wa Tundu Lissu kuhusu tukio la mbunge huyo wa Singida Mashariki kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30, nje ya nyumba aliyokuwa akiishi jijini Dodoma Septemba 7, 2017


Arusha. Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ametilia shaka maelezo ya Adam Bakari, dereva wa Tundu Lissu kuhusu tukio la mbunge huyo wa Singida Mashariki kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30, nje ya nyumba aliyokuwa akiishi jijini Dodoma Septemba 7, 2017.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Februari 13, 2019 jijini Arusha, Lugola amesema maelezo ya dereva huyo yanatia shaka, wanataka awaeleze mambo kadhaa yatakayosaidia uchunguzi wa tukio hilo.

Amesema wanamtaka awaeleze kwa nini alipoona wanafuatwa na magari mengine nyuma akiwa pamoja na mbunge huyo wa Singida Mashariki (Chadema), hakuchukua uamuzi wa kwenda kituo cha polisi kilichopo jirani ya nyumba aliyokuwa akiishi Lissu.

Lugola amesema dereva huyo anapaswa kueleza iweje Lissu apigwe risasi nyingi na yeye asipatwe na risasi hata moja wakati katika gari walilokuwa alikuwa ameketi upande wa kulia.

"Kwa hali ya kawaida ni jambo la kushangaza risasi zote hizo wanasema 38, hata moja haikumpata dereva huyu,” amesema Lugola.

Waziri huyo pia amehoji risasi hizo kutoharibu kisanduku kilichopo katikati ya gari hilo sehemu ya mbele, kinachotenganisha dereva na abiria.

Kuhusu eneo hilo kuondolewa kamera za CCTV, Lugola amesema nyumba za Serikali jijini Dodoma hazina kamera hizo.

“Huu ni upotoshwaji mkubwa ambao unalenga kuwadanganya wananchi na kuwataka waichukie Serikali yao na Rais John Magufuli na mimi kama waziri wa mambo ya ndani sitokubali,” amesema.

Amebainisha kuwa eneo alilokuwa akiishi mbunge huyo linalindwa na askari wa kampuni binafsi za ulinzi, si polisi na kubainisha kuwa kutokana na utata huo ndio maana wanamtaka mbunge huyo na dereva wake kutoa maelezo kukamilisha upelelezi.

“Wao ndio walikuwepo watuambie hawa waliompiga risasi ni wanawake au wanaume, ni wanene au wembamba, warefu au wafupi,” amesema.