Lukuvi: TTCL, Tanesco wadaiwa sugu kodi ya ardhi

Wadau wa umiliki wa ardhi wakimsikiliza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alipokuwa akitangaza taasisi, mashirika na kampuni yanayodaiwa kodi ya pango la ardhi, jijini Dodoma, leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ametaja taasisi, mashirika na kampuni zinazodaiwa mabilioni ya kodi ya ardhi na Serikali ya Tanzania.


Dar es Salaam. Dawa ya deni kulipa. Ndivyo unavyoweza kusema ukimsikiliza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akitaja taasisi, mashirika na kampuni zinazodaiwa kodi ya ardhi, kuzitaka kulipa kabla ya Juni 21, 2019.

Amezitaja taasisi hizo leo Jumanne Juni 11, 2019 katika  mkutano na wakuu wa taasisi, mashirika na kampuni zinazodaiwa kodi unaofanyika mkoani Dodoma.

Huku akieleza jinsi deni hilo lilivyopaa na kufika Sh200 bilioni, Lukuvi amesema Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) linadaiwa Sh40 bilioni na kufuatiwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) linalodaiwa Sh25 bilioni.

“Naomba niwataje wadaiwa, kwanza nianze na TTCL, yupo TTCL humu? TTCL unadaiwa Sh40 bilioni, wa pili ni  Tanesco wewe Tanesco Serikali inakudai Sh25 bilioni,” amesema Lukuvi.

Mbali na TTCL , Tanesco pia wamo Narco, NBC, SUA, TIC, TAA, TRC na nyinginezo.