Lukuvi awasimamisha wawili, ateua wenyeviti 20 mabaraza ya ardhi

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,  William Lukuvi

Muktasari:

Katika kudhibiti nidhamu ya watumishi wa umma, Waziri Lukuvi amewachukulia hatua wenyeviti wawili wa mabaraza ya ardhi huku akiteua wengine kusaidia kutatua migogoro inayojitokeza

Dodoma. Kutokana na malalamiko aliyoyapokea, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amewasimamisha kazi wenyeviti wawili wa mabaraza ya ardhi na nyumba wa wilaya za Karagwe na Kibaha.

Licha ya kuwasimamisha wenyeviti hao wawili, waziri  amewateua wenyeviti wa mabaraza 20 nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Mei 7, 2019 mkoani Dodoma, Lukuvi amesema huo ni mkakati wa kuimarisha mabaraza 97 yaliyopo nchini.

Wakati wizara ikiwa na mkakati huo, Waziri amesema katika kusimamia nidhamu ya uendeshaji na usimamizi wa mabaraza hayo, amekuwa akipokea tuhuma nyingi za rushwa, utendaji mbaya na malalamiko ya wananchi kwa wenyeviti wa Karagwe na Kibaha.

“Kwa mamlaka niliyonayo, nimemuagiza katibu mkuu kumsimamisha kazi Rugate Assey wa Karagwe na Jerome Njiwa wa Kibaha kuanzia leo ili kupisha uchunguzi. Nitaunda tume kuwachunguza,” amesema Lukuvi.

Mbunge huyo wa Isimani, amesema malalamiko aliyoyapokea kutoka kwa wananchi, viongozi wa Serikali wakaandika hata alipowatembelea aliambiwa.

Migogoro ya ardhi nchini ipo maeneo mengi ikiwahusisha wananchi kwa wananchi, wakulima na wafugaji, wafugaji na hifadhi za taifa, kijiji na kijiji hata mkoa na mkoa.