Lukuvi azindua mpango wa ardhi wenye tija kwa wananchi

Muktasari:

  • Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi leo Jumamosi amezindua mpango wa kutambua na kusajili kila kipande cha ardhi mijini ili kuongeza usalama wa miliki ya ardhi na kuwainua wananchi kiuchumi.

Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wiliam Lukuvi amezindua rasmi mpango wa kutambua na kusajili kila kipande cha ardhi mijini ili kuongeza usalama wa miliki ya ardhi na kuwainua wananchi kiuchumi.

Mpango huo wa nchi nzima ambao umeanza katika jiji la Dar es Salaam, utasaidia mmiliki wa eneo kupata leseni ya makazi katika mitaa yote kwa kushirikiana na wenyeviti wa serikali za mitaa.

Akizungumza baada ya uzinduzi huo uliofanyika leo Jumamosi Machi 16, 2019 Waziri Lukuvi amesema baada ya mwananchi kuridhia atapimiwa eneo lake na taarifa zake zitahifadhiwa kielektroniki na atalipia Sh5,000.

Aidha amefafanua maeneo hatarishi yakiwemo yale ya barabarani, maeneo ambayo limepita bomba la mafuta hayatasajiliwa wala kupewa leseni.

Lukuvi amesema mpango huo utaondoa ukuaji wa miji kiholela, utazuia misongamano ya ujenzi.

Pia, amesema leseni zitakazotolewa zitamsaidia mwananchi kupata huduma nyingine za kifedha lakini pia leseni hiyo itakuwa kama dhamana mahakamani.