MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SCOLASTICA: Kesi ndani ya kesi yaibua mambo mazito

Moshi. Maelezo ya ungamo ya mshitakiwa wa kwanza, Hamis Chacha aliyoandika kwa mlinzi wa amani, Irene Mushi yameibua kesi ndani ya kesi licha ya Irene kudai yalitolewa kwa hiyari.

Hayo yamebainika katika kesi ya mauaji ya mwanafunzi wa kidato cha pili wa Shule ya Scolastica, Humphrey Makundi inayowakabili mmiliki wa shule hiyo, Edward Shayo, mwalimu Laban Nabiswa na mlinzi, Hamis Chacha.

Irene, Hakimu Mahakama ya Mwanzo Moshi, ndiye shahidi wa kwanza katika kesi ndani ya kesi.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali mkuu, Joseph Pande kutoa ushahidi juzi, Irene alidai mshitakiwa alifikishwa mbele yake na Inspekta Tenga Novemba 20,2017.

“Wakati naongea naye alikuwa na afya nzuri, nilimuuliza alipigwa akasema ndio alipigwa na polisi wengi tarehe 17.11.2017 baada ya maelezo yake kutofautina na yale ya mlinzi mwenzake,” alieleza.

“Nilimuuliza aliumizwa sehemu gani alinionyesha mgongoni alama ya kuumia. Baada ya kuandika maelezo yake nilimsomea, kisha na yeye akayasoma mwenyewe.”

Shahidi aliomba mahakama ipokee maelezo hayo kama kielelezo, na Wakili David Shillatu anayemtetea mshitakiwa hakupinga.

Baada ya kupokewa kwa maelezo hayo, Wakili Pande alimtaka shahidi kusoma maelezo hayo mahakamani, na aliyasoma neno kwa neno na sehemu waliyoweka saini zao.

Katika maelezo hayo yaliyopokewa kama kielelezo cha kwanza, Chacha anadaiwa kueleza hatua kwa hatua namna alivyompiga panga mwanafunzi huyo hadi kumuua.

Baadaye alimpigia simu mwalimu Laban na baadaye mtu aliyemuita Mzee Shayo ambao walifika eneo la tukio na Mzee Shayo aliamuru mwili huo utupwe mtoni akiamini atakuwa ni kibaka.

Chacha ananukuliwa akidai siku ya Ijumaa (hakutaja tarehe), alikamatwa na mlinzi mwenzake saa 11 jioni na kupelekwa Polisi Himo.

Baada ya kutoka Himo, saa 1 usiku alipelekwa kituo cha Kati Moshi Mjini na hapo alipigwa na polisi wengi ili atoe maelezo kwa madai alitofautiana na mlinzi mwenzake.

Baada ya ushahidi huo, mawakili wa utetezi Elikunda Kipoko, David Shillatu, Wakisa Sambo na Patrick Paul walimhoji shahidi na mahojiano hayo yalikuwa kama ifuatavyo:-

Wakili Shillatu: Ni Kweli hauna diploma, cheti wala digrii ya udaktari?

Shahidi: Ni kweli

Wakili Shillatu: Kwa hiyo ulivyokuwa unaeleza afya ya mshitakiwa ulikuwa unaeleza uongo?

Shahidi: Hapana mtu ukimwangalia tu unajua kama ana afya nzuri

Wakili Shillatu: Ni kweli mshitakiwa wa kwanza alikueleza alipigwa na polisi wengi.

Shahidi: Kweli kwa maelezo yake

Wakili Shillatu: Kwa hiyo shahidi, mtuhumiwa aliyepigwa na polisi wengi ni dhahiri aliumia?

Shahidi: Aliumia sehemu mbili.

Wakili Shillatu: Ni kweli mtu anayepigwa na polisi wengi anaumia au haumii?

Shahidi: Inategemea

Wakili Sambo: Iambie mahakama wewe ni mwanasheria?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili Sambo: Unafahamu lugha ngapi vizuri?

Shahidi: Kiswahili, Kiingereza na Kichaga.

Wakili Sambo: Unafahamu kitu kinaitwa Psychological torture (mateso ya kisaikolojia)?

Shahidi: Nilishawahi kusikia

Wakili Sambo: Unaelewa maana ya mtu kuumizwa kisaikolojia?

Shahidi: Ninaelewa.

Wakili Sambo: Na ni kweli kuumizwa kisaikolojia hakuonekani kwa macho ya binadamu?

Shahidi: Ni kweli.

Wakili Sambo: Ni kweli alipokuwa katika chumba chako alikuwa anaona askari nje?

Shahidi: Ni kweli alikuwa anajua kwa sababu ndio waliomleta.

Wakili Sambo: Kama angekuwa kaumizwa uume angekuonyesha?

Shahidi: Ndio

Wakili Sambo: Kama angeumizwa makalio angekuonyesha?

Shahidi: Ndio angenionyesha

Wakili Sambo: Ni mara ngapi umeshaona sehemu za kiume za watu wanaokuja kutoa maungamo?

Shahidi: Mimi Sijawahi

Wakili Kipoko: Umesema alikueleza kuwa alipigwa na polisi

Shahidi: Ni mshitakiwa alisema

Wakili Kipoko: Na alama za vipigo uliziona

Shahidi: Ndio

Wakili Kipoko: Walimpiga wakati wakichukua maelezo yake?

Shahidi: Ni kweli

Wakili Kipoko: Na walimleta kwako tarehe 20.11.2017 ili atoe maelezo kwako?

Shahidi: Ni kweli

Wakili Kipoko: Alipolalamika kuwa alipigwa, wewe kama mlinzi wa amani ulichukua hatua gani?

Shahidi: Sikuchukua hatua kwa sababu sina mamlaka hayo zaidi ya kuchukua maekezo ya ungamo.

Wakili Patrick: Aliyemkamata mshitakiwa wa kwanza ni nani?

Shahidi: Ni mlinzi mwenzake

Wakili Patrick: Ulipokuwa unahojiana naye, Inspekta Tenga ulikuwa unamuona?

Shahidi: Nilimuona kwa mbali chini ya mti hatua kama 15 au 20

Wakili Patrick: Kwa hiyo Inspekta Tenga alikuwa anaonekana?

Shahidi: Kwa mbali

Wakili Patrick: Ni kweli huko nje kulikuwa na watu wengine?

Shahidi: Walikuwepo watu wachache

Wakili Patrick: Unawafahamu polisi wote wa Moshi?

Shahidi: Siwezi kufahamu wote

Jaji Firmin Matogolo wa Mahakama Kuu anayesikiliza kesi hiyo atatoa uamuzi kama maelezo hayo yapokelewe kama kielelezo ama la katika kesi ya msingi baada ya kumaliza usikilizaji wa kesi ndani ya kesi.

Mwisho