Maalim Seif achambua sakata la Spika, CAG

Dar es Salaam. Zikiwa nimebaki saa 48, Profesa Mussa Assad kuhojiwa na Bunge, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amesema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu huyo wa Hesabu za Serikali (CAG) ameonyesha uungwana mkubwa kwa kutochagua malumbano au ubabe katika kukabili sakata lake.

Maalim Seif amesema hatua ya Profesa Assad kuitikia wito wa Spika Job Ndugai wa kufika mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge Jumanne ijayo ni kuchagua njia ya kistaarabu akisema anaamini watakaomsikiliza hawatataka kumkomoa.

Juzi, Profesa Assad akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam, alisema yupo tayari kuhojiwa na kamati hiyo kama alivyoelekezwa na kiongozi na Spika Ndugai.

Uamuzi wa Spika Ndugai kumtaka CAG kufika mbele ya kamati hiyo kuhojiwa ulitokana na kauli aliyoitoa wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kuhusu kufanyiwa kazi kwa ripoti za ukaguzi zinazotolewa na ofisi yake.

Alisema kushindwa kutekelezwa kwa ripoti hizo huenda kutokana na udhaifu wa Bunge, kauli ambayo, Ndugai alisema ni ya kudhalilisha chombo hicho anachokiongoza.

Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu sakata hilo lilipoibuka Januari 7, Profesa Assad alisema, “Maneno kama udhaifu au upungufu ni lugha za kawaida kwa wakaguzi katika kutoa maoni ya mifumo au utendajikatika taasisi mbalimbali. Kama mmewahi kupitia baadhi ya ripoti zangu, mtaona maneno haya yametumika mara nyingi katika kukazia maudhui mbalimbali ya hoja za ukaguzi.”

Mbali ya Maalim Seif, wananchi mbalimbali walijibu swali kupitia mitandao ya kijamii ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) lililohusu uamuzi wa Spika Ndugai kutangaza kusitisha kufanya kazi na CAG.

Swali hilo lililowekwa mtandaoni juzi lilisema; Nini maoni yako kufuatia kauli ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kuhusu uamuzi wa Bunge kutofanya kazi na ofisi ya CAG sambamba na kuwapeleka wajumbe wa kamati za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac) katika kamati nyingine?

Jana, Maalim Seif ambaye aliwahi kuwa Waziri Kiongozi na baadaye Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SMZ) alisema, “Ushauri wangu kwa Spika, naye afuate njia iliyoonyeshwa na Profesa Assad.

Maelezo hayo ya Maalim Seif yanaunga mkono yale ya Mbunge wa Kigoma Mjini, ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ambaye juzi alisema hatua ya Profesa Assad kukubali wito huo ni kwa sababu ni mtu muungwana asiyependa ugomvi.

“Acha yeye aendelee na uungawana wake, lakini sisi tunalinda Katiba na bado tunaendelea na jitihada za kufungua kesi na ikifanikiwa na kupangiwa majaji CAG hatokwenda bungeni,” alisema Zitto ambaye ni pia ni Kiongozi wa ACT-Wazalendo.

Maoni ya wananchi

Katika maoni yake mtandaoni, Khamis Usanga ameandika, “Anamuita CAG kwenye kamati yake ya haki ili aje ajieleze, sasa mbona anamhukumu kabla ya kuhojiwa? Nafikiri atumie tu busara aepuke jazba, wote wanajenga nyumba moja, kwa nini wagombee fito. Malizeni hili suala kiutu uzima bila watoto kujua.”

Lucas Chambalo ameandika kuwa Spika Ndugai hawezi kukataa kufanya kazi na CAG, bila kufuata taratibu za Bunge za kushirikisha kamati zake akimtaka ajiuzulu.

Mchangiaji mwingine, Rwiza Anthony ameandika, “Hakuna sheria inayosema Bunge lisifanye kazi na CAG.”

Jackson Boaz ameandika, “Tunaunga mkono dhana ya kutokubali Bunge kudharauliwa. Hata hivyo, tunaona sasa unaenda mbali na hili suala. Tunaona ume-overreact.”

Kuwese Mbuya amehoji, “Je, Spika amewashirikisha wabunge wote kuwa wasifanye kazi na CAG au ni uamuzi wake peke yake?”

Mwakabanga Kyonyela ameandika kazi ya CAG ni kukagua hesabu za Serikali na kulikabidhi Bunge na Rais kisha mhimili huo upitie ripoti na kuijadili hivyo uamuzi wake hauna mantiki.

Shepherd Challe amesema Spika anapaswa kuelewa kuwa yupo bungeni kuwawakilisha na kuwatumikia Watanzania na kwamba Bunge ni sauti ya wananchi na kukosolewa ni jambo jema.

Edson Kilalago ameandika, “CAG hafanyi kazi ya Ndugai, anafanya kazi ya Watanzania ambao wanapaswa kujua fedha zao zinatumikaje kwa ustawi wa Taifa hivyo aepuke kuonekana anatumika kuficha maovu.”

Mbali ya wachangiaji hao walioonekana kutomuunga mkono Spika Ndugai, wapo ambao waliungana naye dhidi ya kauli hiyo ya Professa Assad.

Mmoja wao ni, Abdul Sudanis aliyeisema CAG hakupaswa kwenda Marekani na kuitangazia dunia kwamba Bunge ni dhaifu.

“Je, baada ya hapo Wazungu walimzawadia nini baada ya kauli yake? Na je, ubaya wa nchi yako umebadilika?”

Mwingine ni Juma Chillemba aliyendika kwamba wakati umefika kwa CAG kujiuzulu.