Maandamano ya wananchi yamfanya Rais Mnangagwa kuahirisha ziara ya Uswisi

Muktasari:

Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amelazimika kuahirisha ziara yake kwenda Uswisi kufuatia mfululizo wa matukio ya maandamano na vurugu za wananchi wanaopinga ongezeko la bei ya mafuta. Vikosi vya ulinzi na usalama vimekuwa vikipambana na waandamanaji hao kwa wiki moja sasa.


Harare, Zimbabwe. Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amekatisha ziara yake kwenda nje ya nchi kufuatia kuongezeka kwa maandamano ya wananchi yaliyosababisha vyombo vya ulinzi kupambana nao.

Kiongozi huyo alitaka kwenda Davos, Uswisi kushiriki katika Jukwaa la Kiuchumi duniani (WEF) litakaloanza Januari 22–25, mwaka huu kwa lengo la kutafuta fursa za kiuchumi kwa ajili ya nchi yake.

Rais Mnangagwa amenukuliwa leo Januari 21 na shirika la habari la DW akisema kipaumbele chake cha kwanza ni kuifanya Zimbabwe kuwa na utulivu na imara.

Maandamano hayo yalianza baada ya Rais Mnangagwa kutangaza kupanda kwa bei ya mafuta kwa asilimia 150 ikiwa ni moja ya mikakati ya Serikali yake kuinua uchumi wa Zimbabwe. Hata hivyo, wananchi hawakukubaliana na ongezeko hilo.

Akizungumza na gazeti la Serikali la The Herald, Msemaji wa Rais, George Charamba amekilaumu chama cha upinzani cha MDC kwa ghasia hizo zinazotokea kwa kuunga mkono waandamanaji.

“Kiongozi wa MDC amekuwa akisisitiza ujumbe wake kwamba chama chake kitatumia ghasia za mtaani kuyapindua matokeo ya uchaguzi wa mwaka uliopita,” amesema Charamba.

Upinzani nchini humo umepinga uamuzi wa Mahakama uliotolewa Agosti mwaka jana kuthibitisha kwamba Rais Mnangagwa alimshinda mgombea wa MDC, Nelson Chamisa.

Umoja wa Mataifa (UN) umeitaka Serikali ya Zimbabwe kuacha kile ilichokiita matumizi ya nguvu yanayofanywa na jeshi kwa kinachoelezwa kuwa utafutaji wa nyumba kwa nyumba na kwa kutumia silaha za moto.