Madaktari EAC watembelea Taasisi ya Saratani ya Ocean road Tanzania

Mtaalam wa mionzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) Hemed Nyanza akionyesha baadhi ya vifaa vinavyotumika kwenye chumba cha mionzi. Picha na Elizabeth Edward

Muktasari:

Madaktari wa saratani kutoka Afrika Mashariki wametembelea Taasisi ya saratani ya Ocean road nchini Tanzania ambapo watajadili namna ya kukabiliana na changamoto zinazokwamisha matibabu ya ugonjwa huo


Dar es Salaam. Madaktari wa saratani kutoka nchi za Afrika Mashariki wametembelea Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) nchini Tanzania kuona namna inavyotoa matibabu kwa wagonjwa inavyowahudumia.

Ziara hiyo iliyofanyika leo Alhamisi Juni 20, 2019 inakwenda sambamba na mkutano wa siku mbili ni mwendelezo wa jitihada za nchi za Afrika Mashariki kuboresha matibabu ya ugonjwa huo unaogharimu maisha ya watu wengi.

Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk Julius Mwaiselage ameeleza pamoja na kutembelewa na madaktari hao kutoka nchi za Kenya, Rwanda, Uganda, Ethiopia na Tanzania watajadili kwa pamoja changamoto zinazokabili utoaji wa matibabu ya ugonjwa huo.

“Tumekutana hapa kujadili changamoto na mafanikio na kuona ni namna gani tunaweza kuboresha matibabu ili kupunguza idadi kubwa ya wagonjwa wa saratani kutoka katika nchi zetu kwenda India,” amesema

“Tuna changamoto ya dawa kupatikana kwa gharama kubwa na hii ni kwa sababu kila nchi inanunua kivyake lakini tukiunganisha nguvu na kuchukua hizi dawa kwa pamoja gharama itakuwa nafuu, hilo na mengine mengi ni miongoni mwa mambo tutakayoyajadili,” amesema Dk Mwaiselage

Kwa upande wake Mkurugenzi wa taasisi ya Novartis ya Kenya, Dk Nathan Mulure amesema kuendelea kuongezeka kwa wagonjwa wa saratani kunawapa wakati mgumu watoa huduma kutokana na uchache wao.

“Kesi za saratani zimekuwa nyingi sana, halafu tatizo wengi wanafika hospitali wakiwa katika hatua za mwisho hii inatupa wakati mgumu madaktari ukizingatia tuko wachache hivyo tunashindwa kutoa uangalizi wa karibu kwa mgonjwa,” amesema Dk Mulure