Madereva magari binafsi wanaongoza ajali kwa ulevi

Friday October 5 2018

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Bagamoyo. Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limesema madereva wa magari binafsi wanaongoza kwa ajali zitokanazo na ulevi, takwimu za miaka 12 zabainisha.

Hayo yanatokea wakati takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zilizotolewa mwaka 2015, zikionyesha kuwa nchi 34 duniani ikiwamo Tanzania, zina sheria za kuzuia kunywa pombe kupita kiasi na kuendesha gari, ambazo zikisimamiwa vizuri zinaweza kupunguza vifo vitokanavyo na ajali kwa asilimia 20.

Hayo yalielezwa jana mjini hapa na mwanasheria wa kikosi cha Usalama barabarani na mwenyekiti wa kamati ya Bloomberg inayosimamia kampeni ya usalama barabarani nchini, Deus Sokoni kuwa jumla ya ajali 2,250 zilitokea nchini kutokana na ulevi kati ya 2006 na 2017, kati ya hizo nyingi zilikuwa za magari binafsi ikilinganishwa na ya umma.

“Ajali 2,250 tumezirekodi kwa kipindi cha miaka 12, hizi ni zile zilizohusisha madereva waliokuwa wamelewa pombe pekee, lakini katika mfululizo huu, madereva wanaoendesha magari binafsi ndiyo wanaongoza kwa ajali za aina hii ikilinganishwa na mabasi ya abiria, biashara na magari ya umma,” alisema Sokoni.

Alisema kwa kipindi chote hicho, adhabu mbalimbali zimekuwa zikitolewa ikiwamo kunyang’anywa leseni, kufikishwa mahakamani na wengine kushushwa daraja kutoka kuendesha basi la abiria.

“Hatuna haja ya kuwasiliana na dereva kama amekutwa anaendesha gari akiwa amelewa, ni kumnyang’anya leseni tu. Kwa hapa Tanzania sheria yetu inataka iwapo mtu ametumia pombe basi akutwe na kiwango cha pombe katika damu kiwango cha 0.05g/dl au 0.08g/dl zaidi ya hapo tunamkamata na anashughulikiwa ipasavyo kwa kuvunja sheria,” alisema Sokoni.

Hata hivyo, alisema takwimu za madereva walevi wanaopata ajali zilianza kupungua mwaka 2013 kutokana na usimamizi madhubuti wa sheria.

Daktari mwandamizi dharura na maafa kutoka Wizara ya Afya, Mary Kitambi alisema wakati wanaunda sheria, inawezekana pombe haikuwa tatizo, lakini kwa sasa wanagundua tatizo, hivyo lazima wahakikishe wanaifanyia kazi.

Alisema mapendekezo mengi yanaelekeza kwenda kwenye kipimo na kiwango cha 0.00g/dl (kutokuwa na kilevi) ili kuondokana kabisa na ajali zinazosababishwa na madereva walevi, wakiamini uamuzi katika uendeshaji, kuchukua tahadhari na mengineyo yatasaidia kuondokana nazo.

“Unajua mtu anapokunywa pombe umakini hupungua, lakini hata kiwango cha pombe kwenye damu kilichowekwa katika sheria, pia kinatofautiana kwa mtu na mtu, mwingine kiwango cha 0.05g/dl kwenye damu kitamchukua na atalewa zaidi, hii inatokana na umbo la mtu, uzito wa mwili, damu na mengineyo,” alisema Dk Kitambi.

Alipoulizwa sababu za kupungua kwa ajali hizo kwa kipindi cha mwaka 2013 hadi 2017, Sokoni alisema ni kutokana na kuongeza tija katika usimamizi wa sheria.

Alisema kikosi cha usalama barabarani kimekuwa kikitoa mafunzo ya mara kwa mara kwa askari lakini akadokeza kwamba kupungua kwa ajali hakutokani na usimamizi wa sheria pekee, bali kuongeza wigo hasa katika utii wa sheria.

“Kundi kubwa la watu linakuwa na utii wa sheria ikishakuwa hivyo, inaongeza umakini katika usimamizi wa sheria, la pili ni usimamizi wa sheria. Wenyewe na tunafanya operesheni mbalimbali za kukamata wanaofanya makosa mbalimbali ya usalama barabarani,” alisema.

Alisema elimu, utii wa sheria na operesheni ndivyo ambavyo vimechangia kuwaondoa madereva walevi barabarani.

Alisema pia ukaguzi wa magari madogo umesaidia kwa kiwango kikubwa na kuongeza jitihada kutasaidia kuondoa ajali hizo.

“Tunafikiri kuongeza jitihada na kila dereva ajue nini anapaswa kufanya ili kutii sheria bila shuruti. Kila mtu atimize wajibu wake kama sheria inavyotaka, hapo tutapunguza ajali,” alisema.

Advertisement