Maduka ya kubadilisha fedha yafungwa Dar, BoT yatoa maelezo

Muktasari:

  • Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeutahadharisha umma juu ya kutumia huduma za kubadilisha fedha zisizo rasmi na kwamba imeanza utaratibu wa kufuta leseni za maduka ya kubadilisha fedha ambayo yanaendesha shughuli hiyo bila kuzingatia masharti ya leseni zao.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeanza utaratibu wa kufuta leseni za maduka yote yaliyokutwa yanaendesha biashara hiyo bila kuzingatia masharti ya leseni baada ya ukaguzi uliofanyika jana Jumatano Februari 27,2019 na kwamba mchakato huo bado unaendelea.

Taarifa ya BoT iliyotolewa leo Alhamisi Februari 28, imesema ilifanya ukaguzi wa kawaida wa maduka ya kubadilisha fedha za kigeni jijini Dar es Salaam na kubaini maduka mengi yanaendesha biashara hiyo bila kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utoaji wa huduma hiyo.

Leo kabla ya saa 6 mchana, Mwananchi imepita katika mitaa ya Kariakoo na Posta na kubaini maduka mengi ya kubadilishia fedha yakiwa yamefungwa huku machache yakiendelea kutoa huduma hiyo kwa watu.  

Taarifa ya BoT iliyotolewa na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Fedha wa benki hiyo, Jerry Sabi inautahadharisha umma kutotumia huduma zisizo rasmi za ubadilishaji wa fedha za kigeni kutokana na hatari mbalimbali, ikiwemo kuibiwa au kupewa fedha bandia.

“Kama ilivyoelezwa katika taarifa za Benki Kuu ya Tanzania Novemba 2018 na Januari 31, 2019, huduma za kubadilisha fedha za kigeni zinaendelea kupatikana katika mabenki na taasisi za fedha nchini kote pamoja na maduka ya fedha za kigeni ya Shirika la Posta Tanzania (TPC),” inasema taarifa hiyo.

BoT imeonya utumiaji wa huduma zisizo rasmi ni kinyume cha sheria za nchi. Imebainisha kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watoaji na watumiaji wa huduma zisizo halali.