Maendeleo Mbeya yamkosha Rais Magufuli

Muktasari:

Rais John Magufuli amesema mkoa wa Mbeya umebadilika kimaendeleo kutokana na wananchi wake kujituma na kufanya kazi vizuri na kuwahakikishia kuwa changamoto zote zilizopo Serikali itaendelea kuzishughulikia.

Mbeya.  Rais John Magufuli amesema mkoa wa Mbeya umebadilika kimaendeleo kutokana na wananchi wake kujituma na kufanya kazi vizuri na kuwahakikishia kuwa changamoto zote zilizopo Serikali itaendelea kuzishughulikia.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo mkoani Mbeya anakoendelea na ziara yake ya kikazi ya siku nane aliyoianza juzi Alhamisi Aprili 25.

Amesema mkoa huo umepiga hatua kubwa kimaendeleo yanayofanywa na wananchi wake ambayo ni pamoja na ujenzi wa nyumba nzuri na kujituma katika kilimo.

“Nimeona mabadaliko ya maendeleo mnayofanya, ni kwa sababu mnajituma  na mnafanya kazi nzuri, mmejenga nyumba nzuri kila mahali nilipokuwa naangalia naona nyumba za bati, nimeona mazao mnayolima, endeleeni ndugu zangu na ninataka niwahakikishie zile changamoto zilizopo Serikali itaendelea kuzishughulikia,” alisema Rais Magufuli.

Alipokuwa eneo la mji mdogo wa Mbalizi akizungumza na wananchi, alimpa mwezi mmoja Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa kuhakikisha amemaliza tatizo la maji katika mji huio.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo baada ya Katibu wa CCM Wilaya ya Mbeya, Dk Sadakati Kimath kumuelezea kero inayowakabili wananchi wa mji huo kwa miaka mingi kuwa ni  tatizo la upatikaji wa maji safi ya bomba.

“Tatizo linalosumbua mji wa Mbalizi ni mtandao wa miundombinu ya maji ambayo inatusumbua hadi kwenye Ilani ya CCM ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015,” amesema.

Baada ya kutoa kero, Rais Magufuli alimtaka Profesa Mbarawa kujibu kero hiyo na kueleza lini atamaliza kero  hiyo.

Profesa Mbarawa alisema tatizo hilo linafahamika na maji yanayotumika katika  mji huo yanatoka Mbeya Mjini lakini wameanza utekelezaji wa mradi mkubwa utakaogharimu Sh 3 bilioni ambao ndiyo utakuwa suluhisho la changamoto hiyo.

Alisema mradi huo utatekelezwa na wataalamu wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Mbeya (Mbeya-WSSA) na wataanza baada ya wiki tatu kutoka sasa huku akisisitiza kwamba hawatawatumia wakandarasi kwa madai watachelewesha ujenzi wake .

Hata hivyo,  Rais Magufuli alimtaka kuhakikisha mradi huo unakamilika ndani ya mwezi mmoja badala ya wiki tatu za Profesa Mbarawa.

Alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila kufuatilia na kuhakikisha watalaamu wa Mbeya-WSSA wanapewa Sh3 bilioni ili utekelezaji wa mradi huo uanze na akaahidi kufuatilia kwa karibu ili kujua maendeleo yake.

“Kwa miaka mingi tangu uhuru wananchi wamekuwa wakisikia maneno ya kisiasa na ahadi lakini sasa wamechoka, Waziri (Profesa Mbalawa) ameahidi wiki tatu lakini mimi ninamuongezea mwezi mmoja ili akamilishe mradi huu na muanze kupata huduma safi ya maji ya bomba,” amesema.

Akiwa eneo la Mafyati, Rais Magufuli alisema suala la maendeleo halina chama na yeye anawatumikia wananchi wote huku akisema anawapenda wananchi wa Mbeya.