Magufuli: Niliogopa fedheha kwenda kuiangalia Stars

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema alilazimika kuangalia mechi kati ya Tanzania na Uganda nyumbani kwa sababu aliogopa kupata fedheha uwanjani endapo wangefungwa
  • Tanzania imefuzu kucheza michuano ya soka Afrika (Afcon) nchini Misri mwaka 2019 baada ya ushindi wa jana wa mabao 3-0 dhidi ya Uganda

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema alilazimika kuangalia mechi kati ya Tanzania na Uganda nyumbani kwa sababu aliogopa kupata fedheha uwanjani endapo wangefungwa.

Ameyasema haya leo Jumatatu Machi 25, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam katika hafla ya kuwapongeza wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ pamoja na bondia Hassan Mwakinyo baada ya kuiwakilisha vizuri nchi katika mashindano.

Amesema wakati akiangalia na Tanzania kuongoza kwa goli moja alifurahi na kusema Watanzania wanaweza huku akiwaza kuwa goli lile litarudishwa ndani ya muda mfupi.

“Mke wangu (Janeth) akawa ananiambia Tanzania leo tunashinda nikamwambia wewe unajua nini, tukawa tunabishana pale, walivyokuwa wanatangaza katika televisheni za Tanzania nikaona wanaweka chumvi nikaweka Supersport na kuona utangazaji wa haki.”

“Nikawa nasikiliza wanavyosifia wachezaji wa Tanzania nikaona basi leo tunacheza vizuri, baadaye penati na baadaye la tatu nikaona hapa tumeshinda sasa kesi ikabaki kuangalia kule Cape Verde mchezo unakwendaje na ulipoisha nikaona tumeshinda,” amesema Magufuli.

Amesema walimu wa timu walipanga vizuri timu na huenda katika mchezo wa Lesotho walidanganyika au walikuwa hawajawafahamu wachezaji wao vizuri.

“Kwa hiyo machungu niliyokuwa nayo na nafikiri ndiyo ya Watanzania, mmeyamaliza jana hongereni sana.”

“Nina matumaini makubwa kama mchezo wa jana mliouonyesha mkiendelea katika mashindano yanayokuja ya Afcon tunaweza kuingia katika robo fainali, nusu na hata fainali tukachukua na kombe,” amesema Magufuli akiizungumzia Stars ambayo sasa imefuzu kushiriki fainali za soka za mataifa ya Afrika (Afcon) 2019 nchini Misri.