Magufuli: Uchaguzi wa Congo DRC ulikuwa wa mfano

Rais John Magufuli akiwa na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Felix Tshisekedi mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Rais John Magufuli amesema uchaguzi wa Congo unapaswa kuingia katika vitabu vya historia kwa sababu ulikuwa huru, amani na kidemokrasia.


Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema kitendo cha wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kumpa dhamana Felix Tshisekedi kuiongoza nchi hiyo kimeweka historia mpya ya kufanya uchaguzi wa amani na demokrasia huku akibainisha kuwa demokrasia inaendelea kuota mizizi Afrika.

Hayo ameyasema leo Alhamisi ya Juni 13, 2019 katika hafla aliyoiandaa kwa ajili ya rais huyo ambaye atakuwa nchini kwa ziara ya siku mbili.

Magufuli amesema tangu nchi hiyo kupata uhuru wake ni mara ya kwanza uchaguzi umefanyika kwa haki, amani na kwa demokrasia ya hali ya juu.

“Nikupongeze wewe pamoja na aliyekutangulia, hakika mmefanya jambo kubwa la kukumbukwa na kuwekwa katika vitabu vya kihistoria, hongereni sana,” amesema Magufuli.

Akizungumzia ushirikiano uliopo kati ya nchi hizo mbili amesema licha ya kuwa hadi sasa wanajeshi 30 wa Tanzania wamepoteza maisha wakati wakilinda amani DRC, lakini bado Tanzania itaendelea kupeleka wanajeshi kuhakikisha nchi hiyo inakuwa salama.

“Kwa jinsi unavyojitahidi kutengeneza amani kwa kuunganisha vikundi mbalimbali ikiwemo kuwafungulia wafungwa wa kisiasa ni hatua nzuri na sisi tutaendelea kukuombea ili amani itengemae kwa sababu siyo kwa ajili yenu tu bali hata nchi za maziwa makuu tutanufaika,” amesema Magufuli.

Amesema anaamini ziara ya rais huyo itazaa matunda na akamtaka kujisikia na amani akiwa nchini.