VIDEO: Magufuli abainisha sababu ya kumng’oa Makamba

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli ametaja mambo matatu yaliyokuwa changamoto katika Wizara ya Nchi katika ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano) akisema hayakutekelezwa kwa ufanisi kwa miaka minne ya utawala wake.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli ametaja changamoto zilizochukua muda mrefu kutekelezwa katika Wizara ya Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano) ikiwa ni siku moja baada ya kumng’oa aliyekuwa Waziri January Makamba aliyeitumikia wizara hiyo kwa miaka minne mfululizo.

Miongoni mwa sifa alizojizolea Makamba katika uongozi wake ni kutekeleza katazo la mifuko ya plastiki tangu Juni 1 mwaka 2019.

Hata hivyo, akizungumza wakati wa kuwaapisha leo Jumatatu Julai 22,2019 George Simbachawene (Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira) na Hussein Bashe (Naibu Waziri-Kilimo), Rais Magufuli amesema katazo hilo lilicheleweshwa.

“Nakumbuka kwenye suala la plastiki lilichukua muda mrefu, mpaka miaka minne. Nikasaini halikutekelezwa, Makamu wa Rais (Samia Suluhu Hassan) akazungumza, halikutekelezwa, Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) akaenda kuzungumza bungeni halikutekelezwa. Mpaka hapa mwishoni nilipotoa amri ya lazima ndipo likaanza kutekelezwa,” amesema Rais Magufuli.

Ametaja pia suala fedha za miradi ya mazingira akisema kuna fedha zinazotolewa na wafadhili lakini hazitumiki vizuri.

Bahati nzuri utajifunza (Simbachawene) kwa Makamu wa Rais, ambaye ni msimamizi mzuri.

“Fedha zinapelekwa kule lakini impact (faida) yake haionekani. Kuna idara ya mazingira fedha nyingi tu zinatolewa na wafadhili, lakini haziwi reflected (haziakisi) kwenye miradi husika. Kuna mradi kule Rufiji wa kupanda mikoko, mikoko haipo,” amesema Magufuli.

Awali, Simbachawene amesema atalishughulikia suala hilo alipopewa nafasi ya kuzungumza.

Kuhusu utendaji wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Rais Magufuli amelalamikia ucheleweshwaji wa vibali vya uwekezaji wa viwanda akitaka wawekezaji wapewe vibali haraka.

“Pasiwe na ucheleweshaji wa vikabali kwa viwanda vyetu, sisi tunataka viwanda. Wawekezaji wasiwekewe vikwazo kwa sababu ya vibali hivi. Ikiwezekana wawekeze kwanza vibali vya NEMC vitakuja baadaye,” amesema.

“Nimekuwa nikizungumza sana katika eneo hili, mpaka uzungumze na ukishazungumza utasikia kibali kitatolewa baada ya siku tano. Unajiuliza kwa nini hakikutolewa miaka mitano iliyopita,” amehoji

Kuhusu Muungano, Rais Magufuli amemtaka Simbachawene asiwe chachu ya kuvuruga muungano.