Magufuli akutana na bosi wa IMF

Muktasari:

  •  Serikali yaahidi kuendelea na mazungumzo na IMF ikiwamo kuwapitisha kwenye miradi ya maendeleo inayofanyika na kutoa msimamo wa kiuchumi, jambo ambalo halikufanyika kwenye taarifa ya shirika hilo iliyovujishwa 

Dar es Salaam. Rais John Magufuli  amefanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Abebe Aemro Selassie.

Wawili hao wamekutana leo Jumatatu Mei 6, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo huku Selassie akisema  aliomba kukutana na Rais Magufuli ili kuzungumza masuala mbalimbali.

Amesema masuala hayo yanayohusu uhusiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na IMF na jinsi shirika hilo linavyoshiriki katika kutoa ushauri wa kiuchumi.

Taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, imeeleza kuwa Selassie ametumia mazungumzo hayo kumpongeza Rais Magufuli na Serikali anayoiongoza kwa juhudi kubwa zinazofanywa kuwekeza katika miradi mikubwa ikiwamo ya miundombinu.

“Kuhusu kuvuja kwa taarifa za ukuaji uchumi, Selassie amesema IMF itatuma timu ya  wataalamu wake watakaokutana na timu ya wataalamu wa Wizara ya Fedha na Mipango wa Tanzania.

“Lengo la kukutana huko ni  kupitia upya maeneo yaliyoainishwa katika matazamio ya ukuaji uchumi ya Serikali ya Tanzania na yale ya IMF,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Selassie amesema yeye na Rais Magufuli wamekubaliana kuwa IMF na Tanzania watabaki kuwa wadau wanaoaminiana.

“Tunaona fursa nyingi na muhimu katika nchi hii ikiwamo mipango mizuri ya Rais Magufuli,” amesema Selassie.

Amesema katika wiki zijazo wataendeleza mazungumzo ya kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu na Serikali ya Tanzania ili kutazama maeneo yote yaliyofanyiwa mageuzi makubwa na kuyawianisha na ukuaji wa uchumi.

Naye Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango amewahakikishia Watanzania kuwa wizara yake imejipanga kutoa ufafanuzi.

“Tutatoa ufafanuzi kwenye maeneo yote yanayopaswa kuwamo katika  taarifa ya IMF ya ukuaji uchumi wa Tanzania ikiwamo utekelezaji wa miradi mikubwa ya kiuchumi.

“Ili uchumi ukue lazima uwe umewekeza na bahati nzuri Rais Magufuli amemueleza mgeni wake jinsi tulivyowekeza kwenye miundombinu hususan ujenzi wa reli ya kati, ujenzi wa bwawa kubwa litakalotoa megawati 2100 za umeme,” taarifa ya Ikulu imemnukuu Dk Mpango.

 

Pia, ameeleza kuwa amemueleza kuhusu miradi ya barabara na viwanda vingi vilivyojengwa na kwamba hayo ndio yanakuza uchumi na wanaamini kabisa IMF hawakuyazingatia wakati wa taarifa ya awali iliyovuja.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi amewatoa shaka wawekezaji kutoka nchi mbalimbali kuendelea kuwa na imani na mazingira ya uwekezaji ya Tanzania.

Pia, Profesa Kabudi amewataka Watanzania kutokuwa na hofu kwamba wawekezaji watapungua kwa sababu wanaendelea kuja.

“Nashukuru  hata wawekezaji wenyewe hawana hofu kwani hata baada ya taarifa hiyo kuvujishwa bado wengi wameendelea kuja na kuonyesha nia ya kufanya kazi na sisi, nashukuru pia IMF kuja kufanya mazungumzo na sisi.

“Hiyo ni dalili kuwa IMF ipo nasi na bado wanaendelea na mazungumzo, wale waliodhani kuna ugomvi kati  ya pande hizo mbili wamekosea na msimamo wa nchi utafahamika baada ya mazungumzo kuanza na kuwapitisha katika miradi mikubwa ya maendeleo inayofanyika,” amesema Profesa Kabudi.