Magufuli atoa neno Ma-RC, DC kuwaweka ndani watu

Muktasari:

  • Rais John Magufuli amesema wakuu wa wilaya wanapaswa kutumia mamlaka yao vizuri ya kuwaweka ndani watendaji, huku akibainisha kuwa mara nyingine maagizo ni bora zaidi.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amewaasa wakuu wa wilaya kutotumia vibaya sheria na mamlaka walizopewa ikiwamo za kuweka watu ndani na kuwatoa wakidai wamejifunza bila kupelekwa mahakamani.

Magufuli ameyasema hayo leo wakati wa kuwaapisha majaji 15 wa Mahakama Kuu na sita wa Mahakama ya Rufani.

Amesema siyo haki na viongozi wengi wamezungumza kuhusu suala hilo na yeye anarudia kwa sababu kama mkuu wa wilaya ana mamlaka hayo na mkuu wa mkoa akiamua kuweka watu ndani itakuwa ni vurugu, huku akibainisha kuwa mambo mengine yanahitaji kutolewa maelekezo tu.

“Kuelekeza kunaweza kuwa na matokeo chanya wakati mwingine kuliko hata kuweka watu ndani,” amesema.

 Magufuli Magufuli amesema ameamua kumtoa katika uongozi aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Mwanga, Aaron Mbogho na kumhamishia katika kitengo cha wadudu kwa sababu yeye ni mtaalamu wa eneo hilo.

Amesema yaliyokuwa yakitokea wilaya ya Mwanga ya kuwaweka watendaji wa Serikali ndani akiwamo katibu tawala, mkurugenzi kila mmoja alikuwa akiyaona huku vurugu zote zilikuwa zikianzia kwa kiongozi huyo.

“Hata katika mazungumzo yake amekuwa akisema yeye ni mtaalamu pekee wa wadudu Tanzania hakuna kama yeye hivyo nikaamua kumpeleka huko huenda atafanya vizuri...” amesema Magufuli.

Akizungumzia wilaya ya Tarime Rais Magufuli amesema kuna changamoto nyingi ndiyo maana aliamua kumuweka  (Charles Kabeho aliyekuwa kiongozi wa mbio za mwenye mwaka 2018) kwa sababu alikuwa akiona jinsi anavyokemea mabaya na kukataa kufungua baadhi ya majengo yaliyo chini ya kiwango.

“Nikaona ngoja nimpeleke huko kwa Wakurya akawakatalie, kwa wakurugenzi kulikuwa na nafasi zilizokuwa wazi na wengi mlikuwa mnakaimu tumeona kazi zenu nzuri hivyo kasimamieni kafanyeni kazi nzuri, kasimamieni mapato,”

“Nchi inahitaji mapato ya kwenda mbele, msiende mkaanze tena mabishano ya mkurugenzi na mkuu wa wilaya, nimeshazungumza kwa baadhi ya halmashauri ambazo kila siku mabishano nimewaacha kwanza nimewaambia wajirekebishe wameanza kufanya hivyo,” amesema

Akitolea mfano wa maeneo hayo kuwa ni Dodoma na Nyasa huku akisema uongozi ni pamoja na kushirikiana.