Magufuli atoa sababu za kutowateua DPP, kamishna wa kazi kuwa majaji

Muktasari:

  • Rais John Magufuli amesema majaji wapya wanatakiwa kutumia vizuri nafasi walizopewa katika kutenda haki kwa wananchi kwa sababu wengi walikuwapo katika orodha ya waliopendekezwa ila wakabahatika wachache

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema wakati wa mapendekezo ya uteuzi wa majaji jina la mkurugenzi wa mashtaka (DPP) pamoja na kamishana wa kazi yalikuwapo lakini aliamua kuachana nayo.

Magufuli ameyasema hayo leo Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa kuwaapisha majaji 15 wa Mahakama Kuu na sita wa Mahakama ya Rufani.

Katika hafla hiyo, pia walikuwapo wakurugenzi 10 wa halmashauri pamoja na wakuu wa wilaya wawili walioteuliwa Januari 27 pamoja na majaji hao.

“Sasa nikawaza DPP (Biswalo Mganga) ndiyo anayepeleka mafisadi mahakamani kwa nini nimtoe, nikaamua nimuache ili aendelee kuwapeleka.”

“Kamishna wa kazi (Gabriel Malata) naye tangu ameingia amekuwa akifanya vizuri kwa sababu kuna watu walikuwa wanapata vibali vya kazi bila kuwa na sifa lakini sasa  hakuna hivyo nikaona hakuna haja ya kuwatoa,” amesema.

Rais Magufuli amesema kazi ya kuwateua majaji hao ilikuwa ngumu hasa katika kuwahamisha watu katika vitengo vyao kuwapatia vitengo vipya kutokana na utendaji wao.

“Ndiyo maana mnaona kuna wengine wana umri mdogo hapa wengine wakubwa hadi wamebakiza mwaka mmoja kustaafu lakini mimi ndiyo mwenye jukumu la kuwaongezea miaka,” amesema Magufuli.

Amesema majaji wana nafasi kubwa ya kuwa vioo kwa jamii inayowatazama hasa wanapopewa nafasi ya kusimamia haki.

“Kazi zenu zina vishawishi vingi, lawama nyingi, inahitaji kumtanguliza Mungu ndiyo maana huwa ninasema kila mara kuwa majaji wanafanya kazi nzuri hasa wanaposimamia haki,” amesema Magufuli.

Akizunguzia kitendo cha ubakaji kilichotokea wilaya ya Mufindi, Rais Magufuli  amesema wakati akiangalia televisheni aliona jinsi kina mama walivyokuwa wakilalamika juu ya kuachiwa kwa mtuhumiwa aliyebaka watoto 11 bila ya kupewa hukumu yoyote.

“Kwa mujibu wa taarifa za kule, amebaka mpaka wamefikia 11 na kuachiwa na Mahakama, vitu kama hivi vinawaumiza Watanzania na mimi nilitoa agizo kwa mkuu wa mkoa kuwa mtu huyo ashikwe tena waanze kusikiliza upya,” amesema.

Amesema huenda suala hilo linashindikana kutokana na kukosekana ushahidi kwa sababu hivi sasa hadi kipimo cha vina saba vinahitajika.

“Najua IGP (mkuu wa jeshi la polisi) yuko hapa atafuatilia vizuri ajue kwa nini ushahidi unaopelekwa unakuwa haustahili na kama unastahili kwa nini hakimu hatendi haki nafikiri jaji mkuu naye atasimamia hilo,” amesema.