Mahakama Kenya yamzuia gavana Waititu kuingia ofisini

Muktasari:

Jumatatu iliyopita gavana Waititu pamoja na mkewe Susan, walifikishwa mahakamani hapo kwa tuhuma za ufisadi wa Sh588 milioni.

Nairobi Kenya, Mahakama Kuu nchini Kenya imemzuia gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu kuingia ofisini kwake katika kipindi chote kesi yake itakapokuwa ikisililizwa.

Jumatatu iliyopita gavana Waititu pamoja na mkewe Susan, walifikishwa mahakamani hapo kwa tuhuma za ufisadi wa Sh588 milioni baada ya kukiuka sheria na utaratibu wa zabuni.

Masharti hayo ni sehemu ya dhamana iliyotolewa na mahakama hiyo ikiwa ni pamoja na kuwasilisha hati yenye thamani ya Sh15 milioni.

Kwa upande wa mkewe, hakimu Lawrence Mugambi alimuachia kwa dhamana ya Sh4 milioni.

Wengine walioshtakiwa katika kesi hiyo ni mkurugenzi wa kampuni ya Testimony Enterprises Limited, Charles Chege ambaye naye ameachiliwa kwa dhamana ya Sh15 milioni.

Jumapili iliyopita gavana Waititu alijisalimisha katika Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Noordin Haji kuagiza akamatwe na kushtakiwa kuhusu utoaji zabuni ya Sh588 kwa njia haramu.

Gavana huyo anadaiwa kutoa zabuni wa barabara kwa kampuni ya M/s Testimony Enterprises ambayo wakurugenzi wake wana uhusiano na yeye. Tayari kampuni hiyo imelipwa Sh147.3 milioni pamoja na Sh74 milioni katika mradi mwingine.