Mahakama kubainisha wajumbe halali Bodi ya CUF

Muktasari:

  • Kesho Jumatatu, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam itatoa uamuzi wa wajumbe halali wa Bodi ya Wadhamini wa Chama cha Wananchi (CUF) kati ya makundi mawili ya wajumbe yanayovutana

Dar es Salaam. Ni ama kambi ya Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba ama kambi ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Moja kati ya kambi hizo itatoka mahakamani huku ikiwa na furaha na nyingine ikiwa na huzuni ama machungu, baada ya Mahakama Kuu kubainisha wajumbe halali wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho kati ya makundi mawili ya wajumbe yanayovutana.

Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa kesho Jumatatu Februari 18, 2019 na Jaji Benhajj Masoud wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wakati atakapotoa uamuzi wa kesi inayohusu mgogoro wa wajumbe halali wa bodi ya wadhamini wa chama hicho.

Kesi hiyo namba 13 ya mwaka 2017 iliyofunguliwa na mbunge wa Malindi (CUF) Ally Salehe anayetoka kambi ya Maalim Seif, anayewakilishwa na mawakili Mpale Mpoki na Fatma Karume; dhidi ya Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (Rita).

Wadaiwa wengine ni wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho kambi ya Profesa Lipumba waliopendekezwa na kuidhinishwa na Rita, ambao ni Peter Malebo, Hajira Silia, Azizi Dangesh, Amina Mshamu, Abdul Magomba, Asha Suleimani, Salha Mohamed, Suleiman Issa and Musa Kombo.

Wengine ni wajumbe waliokuwa wamependekezwa na kambi ya Maalim Seif, walioenguliwa na Rita, ambao ni Abdallah Khatau, Joram Bashange, All Suleiman, Juma Muchi, Mohamed Mohamed na Yohana Mbelwa.

Mbunge huyo anaiomba mahakama hiyo itamke kuwa wapi ni wajumbe halali wa bodi ya chama hicho kati ya makundi hayo mawili, kwa mujibu wa sheria na chini ya Katiba ya chama hicho ya mwaka 1992 toleo la mwaka 2014.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo ya msingi ya uhalali wa wajumbe wa bodi ya chama hicho, upande wa madai uliwaita jumla ya mashahidi watatu akiwemo mlalamikaji mwenyewe (Saleh), ambaye ndiye aliyekuwa shahidi wa mwisho.

Upande wa walalamikiwa wote kwa pamoja uliwaita jumla ya mashahidi saba.

Katika ushahidi wake akiongozwa na wakili wake, Saleh alidai kuwa wajumbe wa bodi ya udhamini wa chama hicho huteuliwa na Baraza Kuu la Uongozi Taifa la chama hicho ambalo wajumbe wake huteuliwa na Mkutano Mkuu.

Alidai wajumbe wa bodi waliteuliwa  mwaka 2014 wanadumu kwa miaka mitano na kwamba mwaka 2016 baraza hilo liliteua wajumbe wa bodi wa kujaza nafasi zilizokuwa wazi na katibu mkuu akawasilisha majina hayo Rita ili yaidhinishwe.

Saleh alidai kuwa alibaini kulikuwa na majina mengine yaliyokuwa yamewasilishwa Rita kusajiliwa kama wajumbe wa bodi ambayo yalipendekezwa na kundi lingine.

“Niliiomba kampuni ya IMMMA (mawakili) ikawaandikia barua kuwaonya Rita kuwa wasifanye usajili wa bodi nje ya katiba ya chama chetu, nao wakajibu kuwa wanayafanyia kazi,” alisema na kuongeza:

“Lakini Juni 12, 2017 Rita wakamwandikia barua kaimu katibu mkuu kumjulisha kuwa wanaitambua bodi (majina ya wajumbe) iliyopelekwa na lile kundi lingine na si yaliyopelekwa na katibu mkuu kujazwa nafasi za wazi.”

Lakini alipoulizwa na wakili wa Profesa Lipumba, Majura Magafu, kuwa nani mwenye mamlaka ya mwisho kuamua kuwa bodi ipi ni halali alijibu kuwa ni Rita.

Mashahidi wawili kambi ya Profesa Lipumba waliieleza mahakama kuwa wajumbe wa bodi waliokuwepo waliteuliwa mwaka 2012 na hivyo muda wao ulikuwa unaisha 2017.

Walidai kuwa mwaka 2017 Baraza Kuu lilifanya uteuzi wa wajumbe wapya na kwamba wajumbe hao ni halali kwa kuwa waliteuliwa na kikao halali kilichokidhi akidi ya wajumbe, akiwemo mwenyekiti wa chama taifa na Kaimu Katibu Mkuu, Sakaya aliyewasilisha Rita.

Walidai kuwa majina yaliyopendekezwa na Katibu Mkuu Kambi ya Maalim, hayakuwa halali kwani yalipendekezwa na kikao kisicho halali kutokana na kutokuwepo mwenyekiti.

Shaihidi wa Rita, Mwakatobe ambaye ni mwanasheria wake, alidai wao hupokea majina yanayopendekezwa na viongozi wa chama na kwamba baada ya kupokea barua mbili tofauti za mapendekezo ya wajumbe walimuuliza Msajili wa Vyama kwa kuwa ndiye hutunza taarifa za vyama.

Alidai kuwa Msajili aliwaeleza kuwa viongozi wa chama hicho wanaotambuliwa ni Profesa Lipumba, mwenyekiti na Magdalena Sakaya, kaimu katibu mkuu na hivyo waliamua kushughulika na barua ya Sakaya kwa kuwa ndiye aliyekuwa ofisini.