Mahakama yaamuru mpagazi aliyeruka dhamana kukamatwa

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa hati ya kukamatwa, mkazi wa Moshi, Dadu Mabula (27) baada ya kuruka dhamana.

 

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa hati ya kukamatwa kwa mkazi wa Moshi, Dadu Mabula (27) baada ya kuruka dhamana.

Mabula ambaye ni mpagazi wa watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro, anakabiliwa na shtaka moja la  kutumia lugha ya matusi kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.

Mpagazi huyo anadaiwa kuandika ujumbe wa matusi katika akaunti ya Facebook inayomilikiwa na kanisa.

Hati hiyo imetolewa leo Jumatano Agosti 14, 2019 na Hakimu Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Maira Kasonde baada ya mshtakiwa huyo kushindwa kufika mahakama kusikiliza kesi yake bila kutoa taarifa.

Kabla ya kutolewa kwa hati hiyo, Wakili wa Serikali, Gloria Mwenda alidai kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kuanza kusikiliza ushahidi lakini mshtakiwa hajaonekana mahakamani wala wadhamini wake, tangu Juni mwaka huu.

 

“Hatuna taarifa za mshtakiwa yuko wapi wala wadhamini wake, hivyo tunaomba mahakama itoe hati ya kumkamata mshtakiwa huyu” alidai wakili Mwenda.

Hakimu Kasonde, baada ya kusikiliza  maelezo ya upande wa mashtaka, amesema mahakama yake inatoa hati ya kumkamata mshtakiwa kwa sababu ameshindwa kufika mahakamani bila kutoa taarifa wala wadhamini wake.

Pia, mahakama hiyo imetoa hati ya kuwaita wadhamini wa Mabula  mahakamani hapo.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Kasonde aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 22, 2019 .

 

Mabula alifikishwa kwa mara ya kwanza Kisutu, Februari 11, 2019 kujibu shtaka hilo katika kesi ya jinai namba 49/2019.

 

Mshtakiwa huyo alikuwa nje kwa dhamana baada ya kudhaminiwa na mdhamini mmoja ambaye alisaini bondi ya Sh 10milioni.

Katika kesi ya msingi, Mabula anadaiwa kutenda kosa hilo katika tarehe tofauti kati ya Januari mosi na Januari 25, 2019, mkoani Kilimanjaro.

Mabula anadaiwa katika kipindi hicho, aliandika matusi katika mtandao wa kijamii wa facebook wa Kanisa la Waadvestista Wasabato (SDA) na hivyo kuzua taharuki kwa waumini wa kanisa hilo.

Kupitia mtandao huo, Mabula anadaiwa kuandika matusi ya nguoni huku baadhi ya maneno yakisomea kama "Biblia ni tamu kusokotea bangi, oya jibebe as jibebe SDA jibebe leo shimo limetema twashinda Bet” kupitia  mtandao wa kijamii wa facebook.