Mahakama yawaita wadhamini wa Lissu

Tundu Lissu


Muktasari:

Wadhamini hao wameitwa na mahakama kueleza hali ya afya yake baada ya Lissu ambaye pia ni mbunge wa Singida Mashariki kutoonekana katika kesi inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imeamuru wadhamini wa Tundu Lissu kufika mahakamani hapo Februari 25 kueleza maendeleo ya afya ya mbunge huyo wa Singida Mashariki.

Wito huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita kudai mbele ya Mahakama hiyo kuwa kesi inayomkabili Lissu na wenzake ilikuja kwa ajili ya kuendelea lakini hadi sasa hawajajua hali ya mshtakiwa wa nne, ambaye ni Lissu inaendeleaje. “Kesi hii imekuja kwa ajili ya kuendelea lakini hadi sasa hatuna taarifa ya hali ya mshtakiwa wa nne (Lissu), tunaamini hata Mahakama hii haina rekodi ya maendeleo yake,” alidai Wakili Mwita.

Hakimu Simba alisema kwa kuwa Mahakama hiyo haina rekodi ya taarifa ya hali ya Lissu zaidi ya kuona kwenye televisheni, Februari 25 wadhamini wake wafike mahakamani hapo ili kueleza maendeleo ya afya yake.

Siku 16 zilizopita, Spika wa Bunge, Job Ndugai alimtaka Lissu kurejea nyumbani kwa madai kwamba hana kibali cha kuwa nje ya nchi.

Spika Ndugai alitoa wito huo baada ya Lissu kutuma taarifa mitandaoni akisema uongozi wa Bunge na Ikulu wanaandaa mkakati wa kumvua ubunge kwa kigezo cha utoro bungeni.

Lissu yupo nchini Ubelgiji akipatiwa matibabu alikokwenda Januari 6 mwaka jana akitokea Hospitali ya Nairobi, Kenya.

Mnadhimu mkuu huyo wa kambi rasmi ya upinzani bungeni alipelekwa Nairobi akitokea Hospitali ya Rufaa ya Dodoma baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 mchana wa Septemba 7 mwaka juzi akiwa katika makazi yake Area D jijini Dodoma akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge vilivyokuwa vikiendelea.

“Yeye ametoka kuugua, aache uzushi arudi nyumbani, tunamsubiri nyumbani. Kitu muhimu ni kwamba ajue hana ruhusa ya Spika ya kuwa huko anakozurura. Sasa achunge kidogo, maana Spika ana nguvu zake, asimpe sababu,” Alisema Ndugai alipozungumza na mwandishi wetu Januari 20, kuhusu kauli yake ya kumtaka Lissu arejee. “Wakati wenzake tuko bungeni tunafanya kazi za wananchi yeye yuko huko, sasa hilo kwa taratibu za kibunge ni kosa. Kwa hiyo arudi nyumbani aache maneno maneno nje huko.”

Alisema hawezi kumpangia Lissu mambo ya kusema ila ajue hana kibali cha kuendelea kuwa nje ya nchi wakati ofisi ya Spika haina taarifa.

Lissu ambaye Desemba 31 mwaka jana alieleza kwamba amehitimisha shughuli za utabibu na sasa anaendelea na mazoezi ya kutembea, hivi karibuni alifanya ziara nchini Uingereza na kufanya mahojiano na Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC). Pia, amefanya mahojiano na vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

Katika mahojiano hayo, mwanasiasa huyo pamoja na mambo mengine aliitaka Serikali kusimamia ulinzi wake pindi atakaporejea nchini. Pia alizungumzia madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu na vyama vya siasa vya upinzani kunyimwa uwanja sawa wa kufanya siasa.