Maisha Mtwara yarejea kawaida

Muktasari:

Baada ya taarifa za Kimbunga cha Kenneth kutua nchini Msumbiji, maisha ya wakazi wa Mtwara yanaendelea kama kawaida

Dar es Salaam. Baada ya kuwepo kwa taarifa za Kimbunga cha Kenneth kutua jana katika mikoa ya Mtwara na Lindi, leo shughuli za wananchi zimerejea kama kawaida isipokuwa wavuvi.

Kimbunga hicho kinadaiwa kupiga Pwani ya Kaskazini ya Msumbiji.

Mmoja wa wananchi wa Mtwara, Aneth Kisika amesema japo jana alikuwa na taharuki lakini leo ameweza kuendelea na shughuli zake kama kawaida.

 “Jana ndio tulikuwa na hofu kubwa lakini leo tumeamka salama na hali ni shwari kabisa nipo kazini na ninaendelea na shughuli zangu,” alisema mama huyo anayefanya biashara ya mitumba mjini Mtwara.

Taarifa zinaeleza kuwa watu waliokuwa wamehifadhiwa kwenye maeneo salama wamerejea kwao na wengi wao wanaendelea na kazi kama kawaida.

“Hakuna mvua wala upepo, hali ya kawaida na watu wanaenda shambani, kazini kwa sababu jana shughuli zote zilisimamishwa,” anasema mkazi mwingine wa Mtwara Arnold Kinaia.

Amesema japo hakukuwa na chakula wala maji yaliyokuwa yameandaliwa kwa wale walioenda kijihifadhi, wanawake wengi walionekana kubeba vyakula kwa ajili ya watoto wao.

Hata hivyo Kinaia ambaye pia ni mvuvi amesema wavuvi wengi hawajaingia baharini wakisubiri taarifa za mamlaka ya hali ya hewa kama kupo shwari.

Mkuu wa wilaya ya Nanyumbu, Moses Machali amesema hali ni shwari na maisha yanaendelea kama kawaida.

“Leo imekuwa kama jana kwa maana kwamba hakuna jua na kuna wingu kidogo na maisha yanaendelea kama kawaida. Wananchi wanaendelea na kazi lakini kwa sababu leo ni siku kuu ya Muungano wafanyakazi hawajaenda kazini,” amesema na kuongeza: “Tunamshukuru sana Mungu kwa sababu ametunusuru katika hili.”