Majaliwa: Ahadi za Magufuli zitatekelezwa kwa asilimia 90 ifikapo 2020

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Muktasari:

  • Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema ahadi zilizotolewa na Rais John Magufuli katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania zitakuwa zimetekelezwa kwa zaidi ya asilimia 90 ifikapo mwaka 2020.

Kilimanjaro. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema ahadi zilizotolewa na Rais John Magufuli katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania zitakuwa zimetekelezwa kwa zaidi ya asilimia 90 ifikapo mwaka 2020.

Amesema Serikali imedhamiria kuwahudumia wananchi na kuhakikisha huduma mbalimbali za kijamii za maji, afya, nishati, elimu na miundombinu zinapatikana kwa uhakika.

Majaliwa ametoa kauli hiyo jana Jumamosi Februari 23, 2019 katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Kituo cha Polisi  cha Tarakea wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro.

Ahadi hizo ni zile zilizotolewa na Rais Magufuli kama Ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020.

Majaliwa amesema mtumishi mzembe, mwizi, mla rushwa na asiyewajibika hana nafasi katika Serikali ya Awamu ya Tano, kutumia fursa hiyo kutoa wito kwa watumishi wote waimarishe utendaji wao.

Amesema kila mtumishi wa umma anatakiwa ahakikishe anafanya kazi kwa bidii ili kuiwezesha Serikali kutimiza lengo lake la kuboresha maendeleo ya wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini hususani vijijini.

“Iwapo watumishi wa umma watatimiza majukumu yao ipasavyo changamoto nyingi zinazowakabili wananchi kama upatikanaji wa maji zitakuwa historia kwa kuwa Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo,” amesema Majaliwa.

Amebainisha kuwa  sasa Serikali inatekeleza kampeni ya Rais Magufuli ya kumtua mama ndoo kichwani, kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma ya maji karibu na makazi yao

Pia, Waziri Mkuu  amewaagiza  viongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Rombo washirikiane na madiwani  wahakikishe wanaboresha masoko katika mipaka ya Holili na Tarakea ili yawe katika viwango vya kimataifa.

Amesema iwapo masoko hayo yaliyo katika mpaka wa Tanzania na Kenya yataboreshwa yatawavutia na wananchi wa Kenya kuja kufanya biashara na kuiwezesha halmashauri hiyo kuongeza mapato.