Majaliwa amsimamisha kazi mhandisi wa maji Same

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi  mhandisi wa maji wa Wilaya ya Same,  Mussa Msangi  kutokana na kushindwa kusimamia utekelezaji wa mradi wa maji Hedaru

Same. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi  mhandisi wa maji wa Wilaya ya Same,  Mussa Msangi  kutokana na kushindwa kusimamia utekelezaji wa mradi wa maji Hedaru.

Pia, amezivunja jumuiya tatu za maji Hedaru na kuagiza viongozi wa wake kukamatwa na kuhojiwa kuhusu mapato yatokanayo na mradi huo.

"Kamanda wa polisi nitafutie viongozi  hawa wa maji walete hapa waniambie kwa nini wananidanganya, utaondoka nao hawa," amesema Majaliwa leo Ijumaa Julai 19, 2019 baada ya kufika eneo la uzinduzi na kukuta maji hayatoki.

Kufuatia hali hiyo Majaliwa pia alimtaka naibu Waziri wa Maji, Juma Aweso kubaki Hedaru kwa siku tatu kuhakikisha anashughulikia changamoto iliyojitokeza katika mradi huo.

Akijitetea, Msangi amesema maji yapo lakini tatizo mradi huo umetumia sola na unapokuwa na mawingu maji wanasumbua, sababu ambayo Majaliwa aliipinga.