Majaliwa awaonya DED, mweka hazina Shinyanga

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa 

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amezindua nyumba 10 za askari polisi katika manispaa ya Shinyanga eneo la Kambarage huku akitumia fursa hiyo kutoa onyo kali kwa mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga na mwekahazina wa manispaa hiyo kuacha kugombana.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ametoa onyo kali kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga (DED), Geoffrey Mwangulumbi pamoja na mwekahazina wa manispaa hiyo, Pascal Makoye na kuwataka wabadilike, watekeleze majukumu yao ipasavyo na waache kugombana.

Taarifa iliyotolewa kwa umma na ofisi ya waziri mkuu imesema Majaliwa ametoa maagizo hayo leo Ijumaa Agosti 9, 2019 wakati akizindua nyumba 10 za askari polisi katika manispaa ya Shinyanga eneo la Kambarage nchini Tanzania.

Amesema viongozi hao wameshindwa kutekeleza majukumu yao ikiwemo kusimamia kikamilifu kazi ya ukusanyaji wa mapato na kuwataka viongozi hao kuacha  kutoa zabuni za ukusanyaji mapato kwa kampuni zisizokuwa na uwezo.

Majaliwa amesema mwaka 2018 walikadiria kukusanya Sh800 milioni  na badala yake walikusanya Sh500 milioni.

“Manispaa hiyo haiwezi kusonga mbele kimaendeleo iwapo viongozi wake hawaelewani, wanagombana kila siku. Mkurugenzi na wenzako nawaonya kwa mara ya mwisho badilikeni na hakikisheni mnatekeleza majukumu yenu ipasavyo yakiwemo ya ukusanyaji wa mapato,” amesema Majaliwa

Kadhalika, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack azisimamishe kazi kampuni zote zilizopewa zabuni ya kukusanya mapato katika manispaa hiyo kwa kuwa zimeshindwa kufanya kazi vizuri na zina madeni.

Akizindua mradi huo wa nyuma za polisi ambao umetokana na fedha kiasi cha Sh225 milioni  zilizotolewa na Rais wa Tanzania, John Magufuli, Majaliwa amesema lengo la ujenzi wa nyumba hizo ni kuhakikisha askari wanaishi katika mazingira mazuri yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yao vizuri.

Waziri Mkuu ametoa wito kwa askari waliopewa funguo kwa ajili ya kuishi katika nyumba hizo wahakikishe wanazitunza vizuri na hata inapotokea wamehamishiwa kwenda katika vituo vingine, wale watakaohamia wakute nyumba hizo zikiwa katika mazingira mazuri.

Pia, Majaliwa amezitaka idara mbalimbali za Serikali ya Tanzania ziendelee na mchakato wa ujenzi wa nyumba zake kwani wakiwa na nyumba nyingi itasaidia kupunguza idadi kubwa ya askari wanaoishi uraiani.

Hayo yamekuja baada ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga (RPC) Richard Abwao kusema awali fedha zilizotolewa zilikuwa zijenge nyumba tisa za vyumba viwili lakini kutokana na ubunifu waliweza kuboresha mradi huo kwa kuongeza nyumba moja sambamba na kuongeza chumba kimoja, hivyo kuufanya mradi huo kuwa na nyumba 10 zenye vyumba vitatu vya kulala.

 Kamanda Abwao amemshukuru Rais Magufuli kwa upendo wake mkubwa kwa Jeshi la Polisi Tanzania kwa kulipatia fedha za kuboresha makazi ya askari.

”Mradi huo umekamilika kwa gharama ya Sh278.5 milioni wastani wa gharama za ujenzi kwa nyumba moja ni Sh27.8 milioni na kiasi cha nyongeza cha Sh53.5 milioni zilitolewa na wadau mbalimbali,” amesema  Abwao