Majaliwa azungumzia Serikali ya Tanzania ilivyoboresha mazingira ya uwekezaji

Muktasari:

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa kauli hiyo bungeni jijini Dodoma, akieleza mlolongo wa mambo ambayo Serikali inayafanya kwa sasa kuondoa usumbufu, kero na malalamiko kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza nchini

Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameeleza mikakati mbalimbali iliyowekwa na Serikali kuhakikisha inakuza sekta ya uwekezaji nchini ikiwamo kuondoa mlolongo mrefu wa wawekezaji kupata maeneo ya kuwekeza nchini.

“Kwenye uwekezaji sasa tumefikia hatua nzuri kwa kutengeneza andiko maalumu ambalo limeonyesha nia rahisi za uwekezaji nchini kwa lengo la kuondoa usumbufu kwa wawekezi wetu na tunatengeneza mazingira rahisi,” amesema Majaliwa leo Alhamisi Aprili 25, 2019 katika maswali ya hapo kwa papo kwa Waziri Mkuu akijibu swali la mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Dk Jasmini Tiisekwa.

Katika swali lake, Dk Tiisekwa amesema Dira ya Maendeleo ya Tanzania ni mwaka 2025 kufikia uchumi wa kati na viwanda ni kigezo kimojawapo, huku akitaka kujua Serikali imeweka utaratibu gani mzuri kwa wawekezaji wa kuwa wengi wanalalamika kukwamishwa na kusumbuliwa.

“Ni kweli nchi yetu imejikita katika kuboresha uchumi wake kupitia viwanda ambavyo tumetoa fursa kwa Watanzania na mtu yeyote kutoka taifa lolote kuwekeza nchini,” amesema Majaliwa na kuongeza:

“Suala la uwekezaji tumelipa nafasi hasa katika viwanda, awali tulikuwa tunatumia taasisi ya uwekezaji nchini lakini Serikali imefanya maboresho makubwa katika uwekezaji kwa kuanzishwa wizara ya uwekezaji ili kusimamia uwekezaji kwa ukaribu zaidi, lengo hapa ni kuondoa usumbufu ambao wanaupata wawekezaji hao.”

Pia, amesema wameboresha Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kuzikaribisha wizara zote zinazoguswa na uwekezaji wa kuwa na watu wao.

“Hapa ni ili mwekezaji anapokuja huduma zote apate palepale kama ni ardhi, Brela, TFDA. Tuna idara 11 pale za kumhudumia mwekezaji,” amesema.

Amesema baada ya wizara hiyo ya uwekezaji kuwa ofisi ya Waziri Mkuu na kusisitiza: “Tumeanzisha mfumo wa kielekroniki ambao mwekezaji anaweza kuomba leseni popote pale alipo. Tunatambua kuna wawekezaji nje ya nchi, hapaswi kuja Tanzania kuomba kupata ardhi au ithibati ya uwekezaji anaweza kujaza kila kitu huko alipo.”

“Tunatengeneza hayo yote kurahisisha mfumo wa uwekezaji kwa lengo la kupanua wigo wa uchumi nchini kulipia viwanda, kilimo, madini na kila eneo ambalo mwekezaji anataka kuwekeza. Tanzania imefungua nafasi na wigo mpana zaidi wa uwekezaji.”