Majarida, magazeti yatakayoshindwa kuhuisha leseni mwisho Machi Mosi, 2019

Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas 

Muktasari:

Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas leo amezungumza na wanahabari mjini Dodoma na kueleza umuhimu wa majarida na magazeti kuhuisha leseni kalba ya Machi Mosi, 2019

Dodoma. Serikali imetoa siku 24 kwa magazeti na majarida yote nchini Tanzania ambayo hayajahuisha leseni zake kufanya hivyo kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Februari , 2019 na msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas jijini Dodoma katika mkutano na waandishi wa habari, kusisitiza kuwa muda huo ukimalizika, watakaokaidi agizo hilo hawataruhusiwa kuchapisha.

Amesema kwa mujibu wa sheria ya huduma ya vyombo vya habari ya mwaka 2016 inawataka wamiliki wa majarida na magazeti kuhuisha leseni zao kila baada ya mwaka mmoja.

“Novemba mwaka jana tulitoa notisi ya kuwakumbusha kuhuisha leseni zao, wapo baadhi walifanya hivyo na wengine hawakutekeleza kabisa,” amesema Dk Abbas.

“Sasa tunatoa tena notisi nyingine ambayo ni ya mwisho hadi kufikia Machi Mosi, 2019  majarida na magazeti yote yawe yamehuisha leseni zao vinginevyo itakuwa ndio mwisho.”

Amewataka viongozi wa umma kutekeleza sheria kwa kutoa habari huku akisema wataanza kuwafuatilia  watendaji wanaokaidi matakwa haya ya kikatiba.

“Hivi karibuni nilifanya ziara mikoa 14 pamoja na kufafanua mambo mbalimbali ya Serikali nilipata wasaa wa kusikiliza kero za wanahabari hasa wengi wakilalamikia ugumu wa watendaji wa Serikali kutoa taarifa za utekelezaji,” amesema.

“Natumia mkutano huu kuwakumbusha watendaji mbalimbali wa Serikali katika ngazi zote kama habari husika haijazuiwa kisheria, wanaweza  kutoa habari na kueleza utekelezaji wa ahadi tulizoahidi ni takwa la katiba na sheria na si utashi mtu binafsi.”