Makamba: Utu wa Ruge unapimwa kwa aliyoyaacha

Muktasari:

Makamba alisema kwamba Ruge hakuwa na vyeo na mali nyingi lakini alipata heshima na ameondoka kabla ya kuyafanya mambo mengi waliyopanga


Dar es Salaam. Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Mazingira, January Makamba amesema utu wa Ruge Mutahaba unapimwa katika yake aliyoacha duniani.

Amesema wengine wanaweza kuwa na vyeo, pesa na mali nyingi lakini asipate heshima kubwa kama aliyoipata aliyekuwa Mkurugenzi wa Vipindi wa Clouds Media, Ruge.

Akitoa salamu za mwisho wakati wa kuaga mwili wa Ruge, Makamba aliwapa moyo wazazi wa Ruge kuwa msiba huo usiwaumize kiasi cha kumkosea Mungu kwa sababu mtoto wao aliishi matendo mema.

Makamba alisema Ruge ameondoka kabla mambo mengi waliyopanga hayajafanyika.

"Nimelia peke yangu, nimelia kwa sababu sijalipa deni kubwa la heshima uliyonipa, ulinipa upendo wa dhati na tulipanga vitu fulani hivi lakini umeondoka kabla hatujafanya, nimechanganyikiwa," alisema.

Kiongozi huyo aliyemaliza hotuba yake kwa kuimba wimbo wa Helo Helo Tanzania alisema Ruge alipenda na aliagiza siku ya kuondoka duniani tuimbe.

"Ndoto na fursa ndio maneno mawili ambayo Ruge aliyapenda, msiba huu umetuunganisha Watanzania bila kujali vyama na msiba huo umetoa fursa ya ndoto yake kudumu," alisema.

Alimtaka kila mmoja kujiuliza bango lake limeandikwaje na litasomekaje wakati akifa.

"Leo tunatua bango la Ruge likisomeka vizuri, jiulize leo ukiondoka bango lako linasomekaje? Sisi kuja kwetu hapa tumekuja kumvisha taji la heshima, wengine tunaweza kuwa na madaraka ya vyeo, pesa nyingi na mali nyingi lakini tusipate heshima hii," alisema Makamba na kuongeza kuwa alama kubwa aliyoiacha Ruge anaishi kwenye mioyo ya watu.

Makamba anasema ukitaka kupima utu wa mtu ni namna wanavyowachukulia watumishi hasa wa ndani. "Mtu anaweza kuwa mwema sana lakini mtumishi wake wa ndani anapewa vyakula vibovu."

Alisema Ruge alifaulu mtihani wa kuweka utu mbele kwa kila mtu. "Ruge alibaki kuwa mtu mwenye moyo mpana wenye nafasi kwa kila mtu, hakuwa tajiri wa moyo

Alikuwa na masikio ya kuwasikia wote, mikono mikubwa ya kuwakumbatia wote na mdomo wa kusikiliza kila mtu," alisema.

Makamba alisema simulizi za maisha zinatengenezwa na mtu mwenyewe wakati wa uhai wake na kuongeza kuwa maisha ni kama bango ambako mtu anapotoweka linaanza kusomeka.