Makonda azungumzia matibabu ya Paschal Cassian

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,  Paul Makonda

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,  Paul Makonda amesema baada ya kutoka kwa majibu ya  vipimo vya mwimbaji wa muziki wa injili,  Paschal Cassian taratibu za kumpeleka nje ya nchi kwa matibabu zaidi zitafanyika

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,  Paul Makonda amesema baada ya majibu ya  vipimo vya mwimbaji wa muziki wa injili,  Paschal Cassian  kutoka, taratibu za kumpeleka nje ya nchi kwa matibabu zaidi zitafanyika.

Kauli hiyo ya Makonda ni mwendelezo wa ahadi zake za kumtibia mwimbaji huyo alizozitoa wiki iliyopita.

Mkuu huyo wa Mkoa ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 21, 2019 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) baada ya kuzungumza na madaktari na kumjulia hali mwimbaji huyo.

Cassian alipata ajali ya gari akiwa njiani kurejea Dar es Salaam akitokea Dodoma katika shughuli zake za muziki na kuumia  sehemu mbalimbali mwilini.

Kwa mujibu wa Makonda, vipimo hivyo ndio vitatoa picha kama atatibiwa nchini au nje.

"Daktari anayemtibia ameanza kufanya mawasiliano na madaktari wenzake waliobobea kutibu tatizo kama la Cassian. Mawasiliano hayo pamoja na vipimo ndiyo yataamua nchi gani anakwenda kutibiwa,” amesema Makonda.

" Gharama zake nafikiri hazitakuwa kubwa nazo zitajulikana  baada ya kila kitu kukamilika.”

Dk Steven Kaali wa  kitengo cha Urolojia anayemtibia Cassian amesema kuwa vipimo vikikamilika watakuwa na jibu kuhusu nini kinaendelea kwenye matibabu hayo.

"Nafanya mawasiliano na tunaendelea na vipimo, leo ni siku ya tatu tangu aanze vipimo, kweli anahitaji matibabu na nia yetu ni kuona hilo linakamilika hapa nchini au nje ya nchi kwa maelekezo ya mkuu wa Mkoa" amesema Dk Kaali.

"Namshukuru Makonda kwa msaada huu, bado nahitaji kuombewa kwa sababu madaktari na vipimo vinaonyesha ninaumwa sana na ninahitaji matibabu ya kina" amesema Cassian.