Makontena ya vigogo hatarini kupigwa mnada

Friday December 28 2018
pic makontena

Dar es Salaam. Makontena zaidi ya 1,000 yakiwamo ya vigogo nchini, yapo hatarini kupigwa mnada na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kama watashindwa kulipia ushuru ndani ya siku 30.

Tangazo la TRA la Desemba 19 lililotolewa kwenye gazeti la Serikali la Daily News, limewataja watu na taasisi maarufu 1,332 zikiwamo kampuni za kitaifa na kimataifa kudaiwa ushuru.

Baadhi ya taasisi hizo ni kampuni ya Kijoti, inayomilikiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo; Inspekta Jenerali wa Polisi; Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP); klabu ya Simba ya Dar es Salaam; kampuni ya Mohammed Enterprises Ltd na kampuni ya Vodacom.

Kukwama kwa makontena hayo bandarini kumekuja ikiwa ni miezi mitatu tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kukumbana na mkasa kama huo baada ya kuagiza makontena 20 yenye samani aliyodai yalikuwa kwa ajili ya shule za mkoa wake.

Makonda alitakiwa kulipa ushuru wa Sh1.2 bilioni jambo ambalo lilikuwa gumu kutekelezeka na baadaye TRA ililazimika kuzigawa samani hizo baada ya minada takribani mitatu kukosa wateja.

Tangazo la Kamishna wa Forodha na Ushuru wa TRA, Usaje Asubisye limeorodhesha mali na wamiliki wake huku likitoa siku 30 kuziondoa.

Advertisement

“Umma unatangaziwa kuwa bidhaa zilizoorodheshwa zitatambuliwa kuwa zimetelekezwa endapo hazitaondolewa kwenye maeneo ya forodha ndani ya siku 30,” linasema tangazo hilo.

Kampuni ya Kidoti inayojishughulisha na urembo, iliagiza kontena namba HJCU2320135 la nywele bandia (hair weaves) na limehifadhiwa katika bandari kavu ya Said Salim Bakhresa.

Alipopigiwa simu kwa namba yake ya kawaida ili azungumzie kontena hilo, Jokate hakupokea na alipopigiwa kwa namba ya kampuni yake, alipokea lakini baada ya mwandishi kujitambulisha, alikata.

Kuhusu makontena mawili ya Jeshi la Polisi yaliyoagizwa kwa jina la Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) yenye vipuri ambayo yamehifadhiwa katika ghala la kampuni ya Ticts, Msemaji wa jeshi hilo, Ahmed Msangi alisema “Sina taarifa hizo, waulizeni wao TRA.”

Alipoulizwa, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA, Richard Kayombo alisema walichokifanya ni kutoa notisi ya wahusika kutoa mizigo yao bandarini na hawezi kueleza zaidi.
“Taarifa zaidi zinabaki kuwa kati yetu TRA na mteja,” alisema.

TRA imeitaja pia klabu ya Simba iliyoagiza makontena matatu yenye vifaa mbalimbali vya michezo na kampuni ya Yapi Markezi inayojenga reli ya kisasa ya Standard Gauge (SGR), yenye makontena ya vifaa mbalimbali vya ujenzi.

Kampuni nyingine ni kiwanda cha Saruji cha Dangote, kiwanda cha Saruji Mbeya na Eco Bank.

Advertisement