Malipo yakwamisha walimu kuripoti shule walizopangiwa

Muktasari:

  • Walimu waliohamishiwa shule mpya wengi wameshindwa kuripoti kwenye shule hizo kutokana na  kutolipwa stahiki zao.

Serengeti.  Halmashauri ya wilaya ya Serengeti mkoa wa Mara imeombwa kuwalipa stahiki zao walimu waliohamishiwa shule mpya za sekondari ili waendelee kufundisha wanafunzi.

Diwani wa kata ya Sedeko wilaya ya Serengeti, Raphael Matiko katika kikao cha baraza leo Jumatano Aprili 24 amesema walimu wengi waliopangiwa shule hizo hawajaripoti vituoni kwa kutolipwa.

"Wananchi wamejenga shule kwa nguvu zao na zimepangiwa watoto lakini walimu hawapo kwenye vituo kwa kuwa hawajalipwa fedha za mizigo,  tunaomba walipwe ili waweze kufundisha," amesema.

Ofisa elimu sekondari wilaya hiyo, William Makunja amesema wanasubiri fedha za ruzuku ili walipe madai hayo.

Naye kaimu mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Rebeca Msambusi amesema ruzuku ya elimu ya sekondari watakayopokea sehemu zitatumika kulipa stahiki zao ili waweze kutekeleza majukumu yao.