Mama afanya mauaji ya kikatili kwa mwanawe, achemsha jikoni mabaki ya viungo

Picha hii sio ya tukio husika.

Muktasari:

  • Polisi mkoani Geita wanamshikilia mama mmoja anayedaiwa kuwa na tatizo la akili kwa tuhuma za kumuua mtoto wake na kumkatakata vipande kisha kuchemsha jikoni.

Geita. Mwanamke anayedaiwa kuwa na tatizo la akili, anashikiliwa  na polisi mkoani Geita kwa tuhuma ya kumuua na kisha kumkatakata vipande mtoto wake aliyekuwa na umri wa mwaka mmoja na nusu, kisha kuchemsha mabaki ya mwili wake jikoni.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Dismas Kissusi ameliambia Mwananchi jana Usiku Juni 22, 2019.

Amesema tukio hilo lilitokea Juni 21, 2019 katika Kijiji cha Buligi, Kata ya Senga wilayani Geita.

Kamanda Kissusi amemtaja mwanamke huyo kuwa ni Happyness Shedrack (36) na kwamba, uchunguzi wa awali unaonyesha ana historia ya kuwa na matatizo ya akili.

Hata hivyo, polisi wanasema wataendelea kumshikilia huku wakiendelea na upelelezi na ukikamilika, watapeleka jalada kwa mwanasheria mkuu wa Serikali kwa hatua zaidi.