MATUKIO: Mambo saba yaliyotikisa Bunge

Dodoma. Wakati hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka wa fedha 2019/20 ikiendelea kujadiliwa bungeni leo, mambo sita yameibuka ikiwamo chombo hicho cha kutunga sheria kusema hakitafanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.

Mengine yaliyotikisa kuanzia Jumanne iliyopita Bunge hilo lilipoanza ni wabunge wa Chadema; Halima Mdee (Kawe) na Godbless Lema (Arusha Mjini) kusimamishwa kuhudhuria mikutano ya Bunge, wapinzani kususia kikao cha Bunge na kutosomwa kwa hotuba yao. Suala lingine ni Spika Job Ndugai kuwazuia wanahabari kuwahoji waliosusia kikao hicho na maoni ya wabunge kuhusu bajeti ofisi ya Waziri Mkuu.

Bunge lilifikia azimio la kutoshirikiana na Profesa Assad Jumanne iliyopita baada ya kumkuta na hatia ya kusema ‘udhaifu wa Bunge’ wakati alipohojiwa na Redio ya Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kutofanyiwa kazi kwa ripoti zake.

Mdee alisimamishwa kuhudhuria vikao viwili kwa kuunga mkono kauli hiyo ya CAG na Lema kwa kuunga mkono kauli ya mbunge huyo wa Kawe.

Uamuzi wa Lema kusimamishwa uliwakera wapinzani walioamua kutoka nje ya ukumbi wa Bunge kabla ya Spika Ndugai kuagiza wasirejee tena bungeni siku hiyo huku akitaka wanahabari wasiwahoji ndani ya viwanja vya Bunge. Pia walishindwa kusoma maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni kuhusu bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu.

Adhabu ya Mdee, Lema

Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini alisema: “Unapomuadhibu mbunge unawanyima wananchi wake haki ya uwakilishi. Unapomuadhibu kwa sababu ya maoni yake, Bunge linaonyesha halina uvumilivu wa kupokea maoni ya upande mwingine.

“Bunge letu ni la vyama vingi, hivyo Spika na wasaidizi wake wanapaswa kulitambua hilo, wasidhani kila kinachosemwa tofauti na maoni yao au viongozi wa Serikali ni utovu wa nidhamu.

“Selasini alisema baba anayewapenda watoto wake hukaa nao, kuwafundisha, kuwaasa na kuwarejesha katika mstari mfano Makinda (Anne, Spika wa Bunge mstaafu), alipata shida sana na mimi aliwahi kuniita akinisihi niongee na wabunge vijana niwaweke sawa.

“Hakuna mbunge aliyefukuzwa wala kuchukuliwa hatua. Bunge la sasa linatumia madaraka yake kwa upendeleo kati ya walio wengi na wachache, lakini taratibu ni walio wachache wasikilizwe na walio wengi wakubaliwe.”

Spika kuzuia wapinzani

Akizungumzia suala hilo, Selasini alisema: “Ni jambo la kushangaza, ni kawaida wabunge wakati kikao cha Bunge kikiendelea kutoka nje na kurudi. Sisi uamuzi wetu wa kutoka ilikuwa kumsindikiza mwenzetu (Lema), tulikuwa tunarejea bungeni lakini tukazuiwa katika ukaguzi tukasikia Spika akitoa tangazo tusirudi. Huwezi kumzuia mbunge kutoka na kuingia bungeni. Ni jambo la ajabu sana na amelianzisha yeye.”

Wanahabari kuzuiwa

Mbunge wa Kaliua (CUF), Magdalena Sakaya alisema: “Sitapenda kuingilia mamlaka ya Spika lakini saa nyingine sijui ni hasira. Wakati mwingine tunatakiwa kufanya uamuzi tukiwa tumetulia, siku hiyo kidogo Bunge lilikuwa na tension (mvutano), uamuzi mwingine unaweza kuwa umetokana na tension na hasira iliyokuwapo, mwisho wa siku tunaweza kuifanya taasisi ionekane inachukua uamuzi wa hasira zaidi kuliko wepesi na hekima.”

Kwa upande wake Selasini alisema “huwezi kuzuia waandishi wa habari wasiwahoji wabunge nini kinaendelea, maana hata wangetuuliza tungewajibu tulikuwa tunamsindikiza mwenzetu na sasa tunarejea kuendelea na kazi nyingine. Siku ile tulikuwa na hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilikuwa lazima turudi bungeni ili kusoma hotuba yetu.”

Kutofanya kazi na CAG

Sakaya alisema: “Niliona Profesa Assad alivyoitwa kuhojiwa na kamati ya maadili nikajua yamekwisha ila kilichotokea kikaoni ndio kimeleta yote haya, labda kama mtu unaweza kuteleza ukisema samahani sikuona kama ni tatizo.”

Sakaya alisema taarifa za CAG hujadiliwa bungeni na mhimili huo huazimia na kutoa maelekezo na mapendekezo kwa Serikali.

“Taarifa za CAG hazifanyiwi kazi maagizo yanayoagizwa na Bunge, lakini CAG anapoleta taarifa nyingine yale ambayo Bunge imeagiza yanakuwa hayajafanyiwa kazi,” alisema Sakaya na kuongeza.

“Kwa mtazamo wangu Bunge tunafanya kwa sehemu yetu, shida kubwa Serikali haiyafanyii kazi yale tunayopendekeza… inawezekana Bunge halijaweza kuisimamia Serikali vizuri kutekeleza wajibu wake, lakini udhaifu mkubwa ninaouona upo serikalini maana ndio ina mawaziri na wataalamu, kama udhaifu upo Takukuru unatakiwa ufanyiwe kazi.”

Alisema wakati Samuel Sitta (marehemu) alipokuwa Spika wa Bunge alikuwa na tabia ya kusamehe wenye makosa.

“CAG ni jicho la Bunge maana anatoa mapendekezo yake, naona tupo njia panda,” alisema.

Naye Selasini alisema azimio la Bunge ilikuwa kutofanya kazi na CAG linatakiwa kuangaliwa kwa umakini.

“CAG ni ofisi sio mtu, unaona tunavyojichanganya. Nadhani viongozi wameona kuna kosa limetokea mahali fulani ndio maana Spika kasema kilichoazimiwa ni kutofanya kazi na Profesa Assad, azimio halikumtaja Assad lilimtaja CAG,” alisema Selasini.

Alisema CAG ndio anasaini taarifa zote za ukaguzi na kubainisha kuwa iwapo zitaletwa bungeni zikiwa na saini yake zitafanyiwaje kazi. “Katiba ni sheria mama, tunajua Bunge na Rais hawawezi kumfukuza kazi CAG. Tumeiweka nchi katika mkanganyiko wa kikatiba. CAG sio mkaguzi tu ndio controller general (mdhibiti mkuu) wa mfuko mkuu wa Serikali, sasa Bunge linakataa kufanya naye kazi, je Serikali nayo itakataa kufanya naye kazi? Na ikikataa mfuko mkuu wa Serikali fedha zitatoka namna gani?” Alihoji.

Wapinzani kutosoma hotuba

“Unapozuia isisomwe unazuia madhumuni ya uwapo wa kambi ya upinzani bungeni kwa sababu haipo kwa ajili ya Mbowe, kwa hiyo huwezi kuzuia kwa kumkwamisha Mbowe na hasara inakwenda kwa wananchi maana madhumuni yoyote yanayowekwa katika mfumo wa nchi na Bunge ni kwa faida ya wananchi, unapozuia ni wazi kuwa unazuia haki ya wananchi,” alisema Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema).

Akizungumzia suala hilo, Sakaya alisema: “Hotuba ya upinzani kutosomwa wananchi wanakosa kusikia upande wa pili maana ripoti ya upinzani ni bajeti mbadala, huanika shida mbalimbali na hata wabunge tunakosa kusikia upande wa pili maana ripoti hiyo haitaweza kujadiliwa. Kutosomwa ni kuwanyima haki Watanzania na wabunge.

“Sasa hivi inajadiliwa upande mmoja tu, mwaka uliopita nakumbuka Mdee (Halima) alirudi bungeni akaomba kusoma bajeti ila hili la sasa, naona alirudi Lijualikali (Peter-Kilombero) lakini sijui kwa nini hakusoma.”

Wapinzani kutoka nje

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Oliver Semuguluka alisema: “Kitendo cha wapinzani kususia kikao na kutoka nje si cha kiungwana kwani wametumwa na watu kuwasemea si kukimbia vikao. Kama kuna mambo yanawakera nashauri wangekuwa wavumilivu mbona muda wa uhai wa Bunge umebaki mchache, wananchi huenda wakawapima kwa hili.”

Hotuba ofisi ya Waziri Mkuu

Katika mjadala wa bajeti hiyo, mbunge wa kuteuliwa, Abdallah Bulembo alitaka makinikia kuruhusiwa kusafirishwa nje ya nchi huku mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe akikosoa utaratibu wa kuwatumia polisi na Takukuru katika ukusanyaji wa kodi.

Wabunge wengine ni Devotha Minja (Viti Maalumu-Chadema) aliyehoji ilipo ndege ya Serikali aina ya Airbus, Tanzania ya viwanda kutokuwa na viwanda vya juisi na maji huku Jafar Michael (Moshi Mjini-Chadema) akisema vitambulisho vya wajasiriamali vinazikosesha halmashauri mapato.