VIDEO: Mauaji ya watoto yamuibua Masauni ataka leseni za waganga wa jadi Njombe zihakikiwe

Muktasari:

Kutokana na malalamiko mengi kutoka kwa waganga wa tiba asili na mbadala, naibu waziri wa Mambo ya Ndani, Hammad Masauni ametaka leseni za waganga wa jadi zihakikiwe upya

 


Njombe. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Hammad Masauni ameuagiza uongozi wa mkoa wa Njombe kufanya uhakiki upya wa leseni za waganga wa jadi ili kujiridhisha uhalali wa mganga husika.

Masauni ametoa agizo hilo leo Jumatano Januari 30, 2019 baada ya kupata malalamiko kutoka kwa waganga wa tiba asili na mbadala wa Mkoa huo katika kikao alichokiitisha na waganga hao ili kutafuta ufumbuzi wa mwendelezo wa matukio ya mauaji ya watoto yanayoendelea wilayani Njombe.

Waganga hao wamemueleza Masauni kuwa kwa sasa kumeibuka utitiri wa watu wanaojitangaza ni waganga wa tiba asili na mbadala waliosajiliwa kisheria lakini si kweli.

 

Mlezi wa Chama Cha Waganga wa Tiba Asili na Mbadala (CCWI) mkoani Njombe,  Antony Mwandulami alisema shida kubwa iliyopo ni kutokuwa na uhusiano mzuri baina yao na Serikali ya mkoa huo ambao wamekuwa wakitoa vibali na leseni za watu wanaoingia ndani ya mkoa.

 

"Huko nyuma kulikuwa na uongozi mzuri, tulishirikiana vizuri kukomesha mauaji kama ya albino hadi mkoa wa Iringa kabla ya kugawanyika na Njombe kukawa hakuna matukio yoyote lakini baadaye kuna kiongozi mmoja wa Serikali hapa Njombe alianza kutuvuruga, akawa anawaruhusu watu kwa kuwasajili kama waganga na tunaamini hawa watu ndio wanaohusika kwa vile hawafahamiki na wenyeji," alisema Mwandulami.

Katibu wa CCWI, Rosta Ndungulu amesema ni vyema viongozi wa Serikali wakajenga ushirikiano mzuri baina yao na waganga wa chama hicho na hata katika suala la usajili wa watu wanaoingia kufanya shughuli ya utoaji tiba asili na mbadala.

Amesema kwa sasa wanatoa leseni hizo kwa kufanya uhakiki wa mtu husika pekee yake badala kushirikisha chama hicho.

Amesema si wote wanaopewa leseni hizo wanakuwa na dhamira ya kutoa huduma inayokusudiwa bali anafanya hivyo ili kuhalalisha uhalifu.

Mganga mkuu wa mkoa wa Njombe, Dk Bumi Mwamasage alisema awali kulikuwapo mgogoro wa kiongozi wa waganga na Serikali lakini aliyekuwa akilalamikiwa alishaondolewa na uongozi wa zamani wa waganga hao waliurejesha ili kuweka mambo sawa.

“Tumeanza kuweka utaratibu mpya kupitia viongozi hawa na Serikali, lakini pia kwa sasa tumesitisha kupokea maombi ya waganga wote wanaotoka nje ya Njombe kuja kufanya kazi zao hapa,” amesema Mwamasage.

Baada ya kusikiliza malalamiko hayo, Masauni amesema alichokibaini ni kukosekana kwa uhusiano mzuri kati ya waganga wa jadi na Serikali.

“Niutake uongozi wa Serikali ya mkoa ufanyike uhakiki upya wa waganga wa jadi kwa kukagua leseni zao lakini pia kutengeneza uongozi mzuri wa watu hawa,” amesema.