VIDEO: Maswali ya Magufuli kuhusu taarifa za polisi kutekwa kwa Mo Dewji

Muktasari:

Rais John Magufuli ameshangazwa na namna jeshi la polisi lilivyoshughulikia tukio la kutekwa mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania, Mohammed Dewji (Mo) akisema kuna maswali mengi hayajapatiwa majibu

Dar es Salaam. Kama ilivyo kwa Watanzania wengi, kumbe hata Rais John Magufuli anajiuliza maswali yaleyale katika sakata la kutekwa mfanyabiashara maarufu nchini , bilionea Mohamed “Mo” Dewji.

Mo alitekwa Oktoba 11, mwaka jana saa 11:00 alfajiri akiwa Hoteli ya Collesum iliyopo Barabara ya Haile Selassie, Oysterbay jijini Dar es Salaam alikokwenda kufanya mazoezi ya viungo. Mfanyabiashara huyo alipatikana Oktoba 20 eneo la Gymkhana, katikati ya jiji.

Mazingira ya kutekwa kwake katika eneo lenye ulinzi mkali wa Serikali na watu binafsi, kamera za usalama na ndani ya eneo la hoteli, pamoja na la kuachwa katikati ya jiji, ambako pia kuna ulinzi mkali, liliibua maswali mengi ambayo Jeshi la Polisi halikuwa kuyatolea maelezo.

Badala yake lilionyesha gari linalodaiwa kutelekezwa na watekaji, silaha zao, nyumba aliyokuwa akihifadhiwa na mtu aliyewaongoza wahalifu hao, bila ya kuwafikisha mahakamani.

Maswali hayo pia yamemshtua Rais John Magufuli na hotuba yake ya jana inaonyesha wenye mamlaka zinazohusika na masuala ya usalama, wamekalia kuti kavu.

Pia kauli ya Rais ina maana Jeshi la Polisi linatakiwa lifanyie kazi suala hilo na mengine ambayo yameacha utata.

Rais alisema hayo jana baada ya kumuapisha Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje iliyokuwa inashikiliwa na Dk Augustine Mahiga ambaye pia aliapishwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria kuchukua nafasi ya Kabudi.

Rais Magufuli alisema kuna kasoro katika utendaji wa Jeshi la Polisi, akiwatahadharisha kuwa Watanzania sasa wanaelewa na wanahoji masuala mengi, akitoa mfano wa sakata la kutekwa kwa Dewji, akisema limeacha maswali mengi ambayo yanahitaji majibu, kwa kuwaWatanzania si wajinga.

Rais aliyataja baadhi ya maswali kuwa ni ilikuwaje mfanyabiashara aliyetekwa, akarejeshwa hadi Gymkhana, halafu watekaji wakaondoka huku wakiacha silaha katika gari lililodaiwa kwamba ndilo lilitumika kumteka na kumrejesha eneo hilo ambalo pia walijaribu kulichoma moto, lakini halikuteketeza.

“Mtu aliyetekwa alikutwa Gymkhana usiku, lakini watu wanajiuliza ‘mh aliendaje pale’. Lakini alipowekwa pale na bunduki zikaachwa pale, unajiuliza huyu mtekaji aliamua kuziacha je angekutana na polisi wanaomtafuta njiani?” alihoji Magufuli.

Pia alisema asubuhi ya siku hiyo Kamanda wa Polisi wa Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa akaonekana “akinywa chai” na aliyetekwa na siku kadhaa baadaye polisi wakaonyesha nyumba alimokuwa akihifadhiwa na watekaji, lakini mmiliki wa nyumba mpaka sasa hajashtakiwa.

“Aliyekuwa anawabeba wale watekaji ni huyu hapa, Watanzania tukawa tunasubiri kwamba huyu sasa ndio atakuwa kielelezo cha kupelekwa mahakamani tusikie kitakachotokea, lakini kimya mpaka leo miezi imepita,” alisema.

Rais alikuwa alionekana akihoji utendaji wa Jeshi la Polisi katika kushughulikia suala hilo ambalo karibu viongozi wote wa juu, akiwamo Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola walilizungumzia tukio hilo kwa nyakati tofauti.

Wengine waliozungumzia suala hilo ni Yusuf Masauni, ambaye ni naibu waziri, Simon Sirro (Mkuu wa Jeshi la Polisi), Robert Boaz (Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai), Jumanne Murilo (aliyekuwa kamanda wa Kinondoni) na Mambosasa.

Akizungumza kwa sauti ya chini, taratibu na upole tofauti na siku nyingine, Rais alisema baadhi ya watendaji wa jeshi hilo hawakutimiza majukumu yao ipasavyo katika kushughulikia suala hilo, lakini hakumnyoshea kidole yeyote kati ya watumishi wa wizara wala polisi.

Katika hotuba yake ya dakika 21 na sekunde 25, Rais alitumia dakika 14 kuzungumzia masuala yanayohusu jeshi hilo akisema ana imani kubwa na polisi na watendaji wake na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, lakini kuna dosari ambazo zinapaswa kufanyiwa kazi huku akitolea mfano wa tukio hilo lililotikisa nchi.

Alisema Watanzania wanajua kuchambua mambo na lilipotokea tukio hilo, zilikuja habari nyingi kwamba waliohusika na utekaji ni Wazungu.

Alisema suala hilo linaacha maswali mengi ambayo hayana majibu huku akisisitiza kuwa mtu aliyekuwa akiwasafirisha watekaji angewataja na Watanzania walitaka kuona huyo mmiliki wa nyumba angalau akijibu.

“Haya hata kama Watanzania watanyamaza, lakini mioyo yao haitakuwa clean (safi). Tukianzisha suala lazima limalizike ili watu wajue matokeo yake,” alisema.

Maswali mengi kuhusu utendaji wa polisi pia yamewahi kuibuka katika matukio kama ya watuhumiwa kuuawa wakiwa mikononi mwa polisi, kutoweka kwa mwandishi wa habari wa Mwananchi, Azory Gwanda mwaka juzi wilayani Kibiti mkoani Pwani.

Mengine ni kutekwa kwa Idrissa Ally (13), Septemba 26, 2018 na Beauty Yohana (3) aliyetoweka Septemba 21. Beauty alipatikana baada ya saa 48.

Matukio mengine ambayo yameacha maswali ni lile la kada wa Chadema, Ben Saanane aliyetoweka Novemba 2017, pia shambulio la risasi la Septemba 7, mwaka huo dhidi ya mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu.

Kauli ya Mambosasa

Kuhusu suala la Mo, kamanda Mambosasa aliiambia Mwananchi jana kuwa hawezi kulizungumzia kwa kuwa maelezo ya Rais ni maelekezo kwa mkuu wa jeshi hilo.

“Kimsingi alikuwa anatoa maelekezo kwa IGP. Jalada la kesi hiyo halipo kwangu lilishakwenda kwa afande DCI (mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai) na likapelekwa kwa state attorney (mwanasheria wa Serikali). Sielewi mimi naweza kusema nini? Lakini mwenye jeshi anaweza kuwa kwenye nafasi ya kulizungumzia vizuri,” alisema Mambosasa.

Mabadiliko ya baraza la mawaziri

Kuhusu mabadiliko madogo ya mawaziri, Rais alisema ni ya kawaida kama ambavyo kocha wa mpira wa miguu anavyoweza kuamua kumchezesha mchezaji katika nafasi yoyote anayoona inamfaa.

“Nilikuwa naangalia kwenye magazeti, wengine wanasema huyu (Mahiga) si mwanasheria, kwani anakwenda kufundisha sheria pale. Wapo mawaziri wengi tu ambao wamekuwepo kwenye Wizara ya Katiba na Sheria ambao si wanasheria, lakini bahati nzuri wizara ile imejaa wanasheria wote,” alisema.

“Hauhitaji wote wawe wanasheria ni vizuri ukapeleka diplomat (mwanadiplomasia) ili wafanye kazi vizuri.”

Alisema Wizara ya Mambo ya Nje inahitaji watu kama Profesa Kabudi wa “kuwasukuma sukuma” ndiyo maana amempeleka mtaalamu huyo wa sheria ili diplomasia iungane na sheria.

Mawaziri walioapishwa

Akizungumza baada ya kuapishwa, Profesa Kabudi alisema huu ni wakati kwa watendaji wa wizara hiyo kubadilika, wasipokubali kubadilika wao ndiyo watabadilishwa.

“Tuna kazi moja ya kufanya mabadiliko ndani ya wizara mara moja na tunaanza na sisi wenyewe. Lazima tubadilike sisi wenyewe. Tusipobadilika tutabadilishwa,” alisema Profesa Kabudi kauli iliyowaacha watu mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo wakicheka.

Kwa upande wake, Dk Mahiga alimshukuru Rais Magufuli kwa kumteua kuongoza Wizara ya Katiba na Sheria ambayo anasema itampa nafasi ya kuwa karibu na familia yake kwa sababu safari zake nje ya nchi zitapungua.

“Katika jumuiya ya kimataifa, vitu havikai bila kubadilika. Unapolinda marafiki, unapotengeneza ubia na ushiriki, lazima uwe macho katika kuwasiliana na kushirikiana na mataifa mengine,” alisema Dk Mahiga akielezea alichokifanya akiwa Wizara ya Mambo ya Nje.

Pia alimuahidi Spika wa Bunge la jamhuri ya Muungano kwamba sasa hatakuwa “mtoro bungeni” kwa kuwa atakuwa hasafiri.