Matumizi chanya ya mitandao yapigiwa debe

Saturday May 25 2019

 

By Mussa Juma,Mwananchi [email protected]

Arusha. Nguvu ya matumizi chanya ya mitandao ya kijamii, imeweza kubadili hali kidemokrasia na kiuchumi katika nchi nyingi za kiafrika hasa kutokana na kuwaunganisha wananchi wa kada zote na ni hatari zaidi kudhibiti mitandao ya kijamii kuliko hata ugaidi.

Hayo yalikuwa miongoni mwa mambo 10 yaliyobainika katika kongamano la vijana juu ya matumizi chanya ya mitandao ya kijamii, lililofanyika jijini Arusha na kushirikisha vijana zaidi 100.

Katika kongamano hilo ulitolewa wito wa kuondolewa vikwazo vya mitandao ya kijamii, kuwepo uhuru wa habari na kuruhusu Bunge Live.

Profesa Azaveli Lwaitama, alisema mitandao ya kijamii,imeweza kushiriki kuleta mabadiliko katika nchi za Sudan, Algeria, Misri, Gambia na Tunisia kwa kuwa ndio eneo pekee ambalo linakutanisha watu wa kada zote.

“Mitandao ya kijamii, haiwezi kudhibitika, unaweza kuzuia kuchapwa gazeti, unaweza kuzuia habari kutangazwa kwenye radio ama runinga lakini si habari za mitandao,” anasema.

Profesa Lwaitama anasema, nguvu ya mitandao ya kijamii imeibainika pia hapa nchini, katika matukio ya kushambuliwa kwa mbunge wa jimbo la Singida mashariki, Tundu Lissu na kutekwa kwa Mdude Nyangali na watu wasiojulikana.

“Kama si kelele za mitandao ya kijamii inawezekana leo Mdude asingekuwa amepatikana lakini pia bila mitandao ya kijamii leo tusingejua nini kilitokea kwa Lissu na ambacho anafanya sasa,” anasema.

Katika kongamano hilo lililofanyika Chuo cha Maendeleo na Uongozi (MS-TCDC), Askofu Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza anasema ni ujinga kudhibiti matumizi chanya ya mitandao ya kijamii.

“Wajinga wengi hujulikana wanapojieleza, ili kuwasaidia hao, inabidi kuwaruhusu waseme ndipo tubaini ujinga wao na kuutafutia tiba. Kuzuia au kudhibiti uhuru wa kujieleza ni kuuwekea mbolea ujinga ambao ni adui wa taifa na utaifa wetu,” anasema.

Askofu Bagonza alisema hoja za wanasiasa na watawala wengi kusema uhuru una mipaka, kimsingi uhuru ukiuwekea mipaka inayoonekana, unakuwa si uhuru tena bali ni utumwa mstaarabu au uhuru wenye mipaka na sio uhuru kamili.

Alisema katika vita dhidi ya umaskini na katika soko huria mitandao ya kijamii, ina nafasi kubwa sana kuchochea mabadiliko katika maeneo hayo.

“Nimeweka ujinga katikati ya umaskini na maradhi kwa makusudi. Sehemu kubwa ya umaskini wetu na sehemu kubwa ya maradhi yetu, vinabebwa na ujinga wetu,” alisema.

Kwa upande wake Rais mstaafu wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Fatuma Karume alisema ni lazima vijana wajue hakuna ambaye ataamua badala yao.

Aliongeza kuwa kama kuna jambo baya linafanyika ni wajibu wao kusema hapana kama ambavyo alifanya Bob Wangwe kwenda mahakamani, kuwapinga wakurugenzi kuwa wasimamizi wa uchaguzi.

Lakini pia alifafanua kuwa siasa si kusema uongo, kwani wanasiasa walio wengi wamekuwa na kauli tofauti, wakiwa majukwaani na maeneo mengine.

“Utakuta mtu unazungumza naye vizuri jambo fulani anatoa maoni mazuri lakini baada ya muda mtu huyo huyo anaongelea tofauti jambo hilo hilo kwa kisingizio ni siasa,” anasema.

Mkurugenzi wa taasisi ya Change Tanzania, Maria Sarungi alisema taasisi hiyo itaendelea kuwatetea mahakamani wanachama wao ambao wanashitakiwa baada ya kutoa maoni kwenye mitandao.

Sarungi alifafanua kuwa ni muhimu maoni hayo yasiwe ni matumizi mabaya ya mtandao kwa kutukana watu ama kuzungumza mambo ambayo ni kinyume cha sheria.

“Tutaendelea kutetea uhuru wa watu kutoa mawazo yao na isiwe kosa ndio sababu sasa tunafungua kesi za kimkakati ili kuruhusu mawazo ya wengine,” anasema.

Advertisement