Mauaji ya watoto Njombe yalivyobadili utaratibu wa maisha ya watu

Njombe. Mji wa Njombe bado upo kwenye giza nene, huku wananchi wakiwa kwenye simanzi kutokana na mwendelezo wa matukio ya mauaji ya watoto wa chini ya miaka 11.

Matukio hayo yalianza kuibuka Novemba, mwaka jana na hadi sasa watoto 11 wamechinjwa kisha kunyofolewa viungo vikiwemo vya sehemu za siri na masikio.

Watoto kadhaa wamenusurika na wengine hadi sasa hawajukalini walipo.

Kwa sasa watu wanalazimika kujifungia kwenye nyumba zao kabla ya saa mbili usiku kutokana na hofu iliyopo, lakini wazazi na walezi wamepata kibarua kipya cha kuwapeleka shuleni na kuwarudisha nyumbani watoto wao, ili kuhakikisha usalama wao.

Katika maeneo mengi yenye mikusanyiko ya watu kwa sasa habari inayotawala ni kuhusiana na mauaji hayo ambayo yanautia doa mkoa huo yakihusishwa kwa asilimia kubwa na imani za kishirikina.

Mkazi wa Mjimwema mjini Njombe, Alanus Haule anasema suala la kutekwa kwa watoto ni aina mpya ya matukio ya kushangaza mkoani humo.

“Kwa sasa familia zetu zinakaa ndani kabla ya saa mbili usiku kwa hofu hii ya kutekwa kwa watoto wetu. (Hii ni) kwa sababu watu halisi wanaojihusisha na unyama huu hawajulikani, hivyo tunajihami wenyewe,” anasema Haule.

Anasema kutokana na matukio hayo imefikia hatua watu kutoaminiana ndani ya jamii, iwe wageni wanaoingia Njombe au hata wenyeji wenyewe kwani suala hilo linahusishwa zaidi na imani za kishirikina.

Baraka Kilumbe, mkazi wa Nazareti anasema, “Watu wengi hususan wafanyabiashara wamekuwa wakitumia njia za kishirikina ili kutafuta utajiri kwa kuua watu wakiwamo ndugu zao ambao huwatoa kafara.”

Anasema miaka ya nyuma mauaji yaliyohusishwa na imani za kishirikina yalikuwepo, lakini hayakuwa katika mtindo kama huu wa kuchinja watoto kisha kuwanyofoa baadhi ya viungo vya miili yao.

Mkazi wa Sido, Philipo Kyalula anasema hivi sasa shughuli nyingi za uzalishaji kwa wazazi na walezi zinakwama kutokana na kazi ya kuwapeleka watoto shuleni na kuwarudisha nyumbani baada ya masomo.

“Hili suala kwa kweli ni zito, tunaacha shughuli za uzalishaji na kugeuka wanafunzi shuleni, maana asubuhi unampeleka mtoto na mchana au jioni unarudi kumchukua,” anasema.

“Lakini vilevile kutokana na hali ilivyo tunalazimika kufunga biashara zetu mapema ili kuwahi kurudi nyumbani, kwanza kwa usalama wetu wenyewe na pili kuimarisha ulinzi wa familia.”

Wageni hatarini

Kutokana na mtandao wa wauaji kutojulikana, kwa sasa wageni wanakabiliwa na hali ya kutoaminika wafikapo katika maeneo yaliyokumbwa na mauaji hayo na hivyo uhai wao kuwa shakani.

Kutokana na hali hiyo, mtu mmoja ameuawa na wengine watatu kujeruhiwa na wananchi katika Kijiji cha Magunguli, kata ya Kibaoni wilayani Mufindi mpakani na wilaya ya Njombe, baada ya kuwahisi watu hao kuwa ni miongoni mwa wale wanaojihusisha na utekaji na kuua watoto.

Watu hao walishukiwa kujihusisha na vitendo hivyo kutokana na ugeni wao kijijini hapo.

Mkazi wa Ikando, Kata ya Kichiwa, Salum Mayemba alisema hivi sasa katika maeneo ya vijijini wageni wanatiliwa shaka na kutokana na mfululizo wa mauaji ya watoto, hasira za wananchi zinaonekana katika maongezi yao.

DC akemea

Mkuu wa wilaya ya Mufindi, Jamhuri William aliliambia Mwananchi kuwa, Januari 31, watu hao walipoingia kijijini hapo wananchi waliwatilia shaka na kutoa taarifa polisi.

Alisema askari walifika kisha wakawaweka chini ya ulinzi kwa mahojiano zaidi.

“Watu hao walipohojiwa na polisi ilibainika ni raia wema tu ambao wamekwenda kijijini hapo kutafuta chakula kwenye moja ya mgahawa na ni vibarua wa mashamba ya chai,” alisema William.

Alisema baada ya kuhojiwa, waliendelea kuwa chini ya uangalizi wa mgambo kwa muda katika ofisi ya kata, lakini wakati huo wananchi wakiwa wameizingira ofisi hiyo kujua hatima ya watu hao.

“Wananchi walipoona hawajui kinachoendelea waliamua kuivamia ofisi hiyo na mgambo walizidiwa nguvu, hivyo wakaanza kuwashambulia watu hao kwa mapanga na mmoja kati yao alifariki (dunia) na wengine hali zao hazikuwa nzuri hivyo wakapelekwa hospitali kwa matibabu.”

Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mikononi mwao, badala yake waviachie vyombo vya ulinzi na usalama vifanye kazi yake.

Kikosi kazi maalumu

Wakati hayo yakijiri, mkuu wa mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka alisema kikosi kazi maalumu kilichotua mkoani humo kufanya uchunguzi wa mtandao unaohusika na mauaji ya watoto, kinahitaji ushirikiano wa dhati.

Mbali na hilo, Ole Sendeka alisema kuanzia sasa yakitokea mauaji watu wa kwanza kukamatwa ni familia nzima ya mtu aliyeuawa na baadaye viongozi wa serikali za mitaa, vitongoji, vijiji na kata.

Aliwataka viongozi kuhakikisha wanafanya uhakiki wa wananchi kwa kuwatambua watu wote katika maeneo wanayoishi na wenyeji wanaopokea wageni wahakikishe wanawatolea maelezo ya kina kwa viongozi wa maeneo yao.

Pia alisema kuanzia sasa mkoa huo umesitisha kupokea waganga wa jadi na wameanza kufanya uhakiki upya wa leseni za wale waliopo.

Mkuu huyo wa mkoa alisema uchunguzi umebaini kuwa matukio yote ni ya kishirikina ambapo watu wanatafuta utajiri kwa kutoa kafara za uhai wa binadamu wenzao, hivyo msako unaendelea kuwabaini wahusika.

Kanisa latoa wito

Jana, Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Njombe, Alfredy Maluma aliwataka viongozi wa dini na madhehebu yote mkoani humo kukemea matukio hayo.

“Suala hili ndugu kama kanisa tunalaani na wote wanaotenda ubaya huu kwa watoto hawa wasiokuwa na hatia damu zao hazitawaacha salama,” alisema Askofu Maluma.