Mazingira mabovu chanzo cha mtoto wa kike kutotimiza ndoto

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe,Jokate Mwegelo (kulia) akimpongeza Mama Fadhila Digodigo aliyefakiwa kumsomesha binti yake hadi Chuo Kikuu. Kushoto ni Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi, Seleman Jafo na katikati ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako. Na Mpiga Picha Wetu

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo alisema jitihada zilizoanzishwa za kupunguza daraja sifuri wilayani Kisarawe zimefanikiwa kwa kiwango kikubwa na matokeo yake yameanza kuonekana.

Dar es salaam. Jamii imetakiwa kupambana na changamoto za mtoto wa kike kwa vitendo na kuwatengenezea mazingira mazuri ili kuwawezesha kutimiza ndoto zao.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako wakati wa harambee ya Tokomeza Zero iliyoandaliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo.

Harambee hiyo imefanyika kwa lengo la kufanikisha ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana wilayani Kisarawe, kununua vifaa vya kujifunzia na kufundishia ili kuongeza kiwango cha ufaulu wilayani humo.

Akizungumza kwa niaba ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan Profesa Ndalichako alisema bado kuna tatizo la ufaulu kwa mtoto wa kike kutokana na majukumu aliyonayo na kutotengenezewa mazingira mazuri yanayosababisha kukatisha ndoto zao.

“Kuna haja ya kutengeneza mazingira mazuri na kupambana na changamoto hizi kwa vitendo,” alisema Ndalichako.

Akizungumzia umuhimu wa harambee hiyo, waziri huyo alisema shule hiyo itakuwa ya mfano na itawasaidia watoto wa kike kupata muda wa kujifunza zaidi na kukwepa vishaswishi vinavyoweza kukatisha masomo yao.

“Malengo ya harambee hii ni ujenzi wa shule itakayokuwa na kidato cha kwanza hadi cha sita, kununua vifaa vya kujifunzia na kufundishia ambavyo vitasaidia kuongeza kiwango cha ufaulu katika Wilaya ya Kisarawe na kuondoa zero,” alisema.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo alisema jitihada zilizoanzishwa za kupunguza daraja sifuri wilayani Kisarawe zimefanikiwa kwa kiwango kikubwa na matokeo yake yameanza kuonekana.

Jafo ambaye pia ni mbunge wa Kisarawe, alisema mwaka 2017 zero zilikuwa 457 na kupitia kampeni hiyo, zimepunguza hadi kufikia 226 mwaka 2019.

Ofisa elimu sekondari Wilaya ya Kisarawe, Patrick Gwivana alisema changamoto wilayani humo bado ni nyingi hasa umbali wa shule za sekondari na makazi ya wanafunzi.

Alisema wengi wao hutembea hadi kilomita 24 hali inayochangia kuwakatisha tamaa na kuamua kuacha shule

“Ndani ya miaka mitano tumekuwa na kesi 106 za watoto wa kike kupata ujauzito ukilinganisha na ufaulu, ndani ya miaka hiyo waliobahatika kwenda kidato cha tano ni 56 tu,” alisema Gwivana.