MABADILIKO: Mbowe kupangua mawaziri vivuli, CUF kutemwa

Dodoma. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni itapangua baraza kivuli la mawaziri ikiwa ni pamoja na kuwaondoa wabunge wa CUF.

Hata hivyo, CUF imesema ikitokea mabadiliko yoyote ya aina hiyo watamuandikia barua Spika kuomba ziwepo kambi mbili za upinzani bungeni.

Kambi ya upinzani imesema itapangua baraza hilo kutokana na mgogoro wa CUF uliosababisha baadhi ya wabunge kumuunga mkono Profesa Ibrahim Lipumba huku viongozi wengine wa juu wa chama hicho wakihamia ACT Wazalendo.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba ametofautiana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vinavyoundwa na Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na CUF.

Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alilieleza Mwananchi jana kuwa anakusudia kufanya mabadiliko hayo. “Nitafanya marekebisho ya baraza la mawaziri na nitalitangaza wakati wowote baada ya kuwa nimewasiliana na Bunge,” alisema.

Awali, katika ufafanuzi wa mabadiliko hayo, kaimu mnadhimu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Joseph Selasini alisema, “kutokana na hali ilivyo ni vigumu kushirikiana nao, ingawa kuna wanaoonyesha nia ya kuendelea lakini ni vigumu.

“Mfano unamteua mtu, au mtu ambaye ana hiyo nafasi akienda kusoma hotuba ya kambi ya upinzani halafu akasimama (Magdalena) Sakaya (naibu katibu mkuu CUF) na kusema kinachosomwa hawakiungi mkono na anaweza kusema hawajamuidhinisha kushika hiyo nafasi.”

Akizungumzia hilo Sakaya, ambaye pia ni mbunge wa Kaliua (CUF) alisema, “Lakini wakileta tatizo lolote sisi tuna haki, tutaandika barua kwa Spika kuwepo kambi mbili. Kwa hiyo stahiki za kambi za upinzani bungeni zitagawanywa mara mbili.”

Alizitaja stahiki hizo kuwa ni mfuko kwa ajili ya wapinzani unaowawezesha kutekeleza mambo mbalimbali ikiwemo kuajiri watu wa kuwaandikia barua.

Katika hilo, Mbowe alisema wanaweza kufanya wanavyotaka, ikiwa kanuni na sheria zitawaruhusu, “Kwani hatuwezi kushirikiana na chama ambacho hakiko katika ushirikiano wetu.”

Msimamo wa CUF

Sakaya alisema msimamo wa CUF ni kuendelea kubaki katika Baraza la Mawaziri Kivuli kwa sababu bado ni wabunge wa chama.

“Kwa taarifa yako wengi wa wabunge wamesharudi katika chama. Mfano kina Bobali (Hamidu-Mchinga), Ngombare (Vedasto-Kilwa Kaskazini) tumeshakaa nao vikao vya chama,” alisema Sakaya.

“Wakati wa mgogoro waliyumba kimsimamo, lakini sasa wamesema wanafuata maamuzi ya mahakama (kumtambua Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti).”

Alisema wanaendelea kuwatambua mawaziri kivuli ambao ni wabunge wa CUF kwa kuwa kambi ya upinzani si hiari ya mtu ila ipo kikanuni na kisheria. Alisema hawategemei wabunge wa Chadema walete pingamizi lolote kuhusu maamuzi ya wabunge walioko katika baraza hilo kufuata uamuzi wa mahakama.

“Wakileta objection (pingamizi) lolote kwamba hawatawatambua basi hiyo kambi itakuwa haina maana. Na sisi tutaomba kwa kuwa kanuni zinaruhusu kuwemo kwa minority (wachache) na majority (wengi) itabidi kuomba ili tuwe na kambi mbili za upinzani bungeni,” alisema.

Hata hivyo, Bobali ambaye ni waziri kivuli wa maji alisema, “kwa sasa naweza kuomba kupumzika nafasi hii kwani nimeipata kutokana na chama na chama kimesema hakishirikiani nao.” “Kwa maana hiyo kama Mbowe atataka niendelee itabidi awasiliane na mwenyekiti mwenzake (Profesa Lipumba),” aliongeza

Akifafanua zaidi Sakaya alisema wakati wa mgogoro wa uongozi CUF, Mbowe alimuondoa kwenye nafasi ya Waziri Kivuli wa Kilimo.

Alisema Mbowe alimwandikia barua Spika akieleza kuwa kwa sababu kuna mgogoro wa chama na yeye (Sakaya) yuko upande wa Lipumba ndio maana anamuondoa, lakini akadai hakuwaondoa wabunge waliokuwa wakimuunga mkono Maalim Seif.

“Nilishindwa ku-react kwa sababu nilikuwa na mambo mengi ya kijimbo na kichama. Nikaona kuwa kiongozi ama si kiongozi hakuna haja ilimradi tu najua mchango wangu unatambulika inatosha,” alisema Sakaya.

Alipoulizwa iwapo kuna ushirikishwaji kwa sasa baina ya vyama hivyo viwili bungeni, Sakaya alisema ana imani wabunge wa CUF wameshirikishwa katika uandaaji wa hotuba mbadala za bajeti kwa sababu hadi sasa hajapokea malalamiko yoyote.

Kuhusu kuunga mkono uamuzi wanayotokana na vyama hivyo ikiwemo kutoka bungeni, Sakaya alisema wakati walipokuwa wakitoka wabunge wote wa upinzani bungeni kama njia ya kuunga mkono mambo mbalimbali walikuwa wanawekeana misimamo.

Alisema hawezi kutoka bungeni kutokana na wabunge wa CUF kutoshiriki katika vikao vya Chadema mara baada ya mgogoro wa CUF kumalizwa na mahakama.

Mabadiliko ya baraza hilo pia yatajaza nafasi za wabunge wengine wa Chadema ambao wamehamia CCM.