Mbunge CCM aipongeza Taifa Stars kufungwa 2-0

Muktasari:

  • Timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ jana Jumapili ilicheza mchezo wake wa kwanza wa Kundio C katika Michuano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) Senegal na kukubali kipigo cha 2-0. Michuano hiyo inaendelea nchini Misri

Dodoma. Mbunge wa Kilolo (CCM) Vicent Mwamoto amewataka Watanzania kutolalamika kwa Taifa Stars kufungwa na Senegal magoli 2-0 na badala yake Serikali kwa kushirikiana na wadau wawekeze kwenye michezo.

Akichangia mapendekezo ya bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ya Sh33.1 trilioni leo Jumatatu Juni 24, 2019 Mwamoto ameipongeza timu ya Taifa Star kwa kufungwa mabao mawili.

Amesema timu ya Senegal ina thamani ya wachezaji wa timu ile ni paundi milioni 380 sawa na Sh1.1 trilioni lakini Taifa Stars thamani yake ni paundi milioni 14 ni sawa Sh 44 bilioni.

“Tusitake kufurahia kwenda peponi wakati tunaogopa kufa maanake ni nini maandalizi ya timu yetu ni bado tunatakiwa tujipange kwa sababu hawa (Senegal) wamewekeza,” amesema.

Amesema wanacheza nchi za nje karibu timu nzima wanarejesha fedha hizo katika uchumi wa Senegal tofauti na Taifa Stars ambayo ina wachezaji wanne tu wanaocheza soka la nje.

“Ushauri wangu kwakuwa uwezekano wakujenga academic ndani ya nchi yetu si rahisi basi tuwatumie wachezaji waliofika nafasi za kimataifa kuwasambaza kwenye shule zote kufundisha michezo baada ya miaka mitatu nchi nzima itabadilika, badala ya kulalamika,” amesema.

Amewataka Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kukuza michezo na si kulalamika wakati hatuchangii katika kukuza michezo.