Mbunge CCM akosoa takwimu wanaopata maji

Muktasari:

  • Mbunge wa Mondoli (CCM), Julius Kalanga amesema takwimu zinazotolewa na watalaamu kuwa asilimia 80 ya watu wanapata maji si za kweli kwa sababu miradi mingi iliyokamilika haizalishi maji

Dodoma. Mbunge wa Monduli (CCM), Julius Kalanga ameitaka Serikali kufanya tathmini ya miradi ya maji nchini ili kupata takwimu sahihi kwa sababu mingi iliyokamilika haizalishi maji.

Kalanga ameyasema hayo bungeni jana Alhamis Mei 2, 2019 akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2019/20.

“Mradi unakamilika leo kesho hautoi maji, kama inatoa maji inatoa kwa kiwango cha chini. Hivi ni taaluma gani ambayo inafanya wasipate maji ya uhakika? Baada ya miezi miwili mitatu mradi kukamilika mradi hautoi maji,”amesema.

Amesema ni muhimu kufanya tathmini ya miradi ya maji nchi nzima ili kufahamu ni miradi mingapi inazalisha maji na ambayo haizalishi, kwa sababu takwimu za wataalamu kuwa asilimia 80 ya watu mijini wanapata maji si za kweli.

“Maana yake wananchi hawapati maji. Tufanye review (mapitio)  ya miradi ya maji ili tupate takwimu za watu ambao wanapata majisafi na salama. Mheshimiwa mwenyekiti hali ni mbaya hasa majimbo ya vijijini naomba Serikali itambue hilo,” amesema.

Amesema kila siku anaona miradi mikubwa inafanyika mijini na kuhoji wanawaweka wapi watu wa vijijini ambao hawana uwezo wa kupata maji safi katika umbali mfupi.

“Hii si sawa,  wafadhili wanatoa fedha mjini sisi tulio vijijini nani mwenye interest na sisi? Hiyo mita 400 kufuata maji mnayoizungumza sisi tunafuata maji kilomita 10 hata wakati mwingine hatupati maji,” amesema.

Ameitaka Serikali kuangalia watu wa vijijini kwa jicho la huruma kwa sababu wanapata shida sana ingawa ndio walipa kodi na waaminifu wakati wa uchaguzi.

“Kama Serikali inasaidia majimbo ya mijini basi ijielekeze kusaidia majimbo ya vijijini. Angalau tukipata maji ndani ya kilomita nne bado ni faida achana na hao wa mjini ambao wanataka mita 400. Mita 400 ndani ya kiwanja chako sisi tunafuata maji kilomita 10 bado maji yenyewe hayapatikani,” amesema.