Mbunge Mollel ataka bunge kumtambua Samatta kwa mchango wake

Muktasari:

Mbunge wa Viti maalum  Amina Mollel amelitaka bunge kutambua mchango wa mchezaji wa taifa Mbwana Samatta na kukemea wanaomwita ni raia wa Kenya.

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu (CCM),  Amina Mollel amelitaka Bunge kutoa tamko la kumpongeza mchezaji wa kimataifa Mbwana Samata kutokana na mchango wake wa timu ya Genk.

Katika mwongozo wa Spika aliouomba leo Jumatano Mei 22,2019 bungeni Jijini Dodoma, mbunge huyo amemtaja mchezaji huyo ambaye ni nahodha wa timu ya Taifa, kama shujaa.

Mollel ameomba mwongozo wa Spika akisema mchango wa Mtanzania huyo unapaswa kuthaminiwa na kujaliwa hata ndani ya Bunge ili kumtia moyo.

Amesema magoli aliyoifungia timu hiyo kwenye ligi ndiyo imewezesha Genk kutwaa ubingwa wa ligi ya Ubergij, amepachika magoli 23.

Hata hivyo, ametaka Serikali kukemea kile kinachoendelea kwenye mitandao kuwa Samatta ni raia wa Kenya akataka jambo hilo lisiachwe tu.

Spika, Job Ndugai amesema Serikali imesikia na jambo hilo ni muhimu, hivyo iangalie namna ya kumtaja shujaa huyo.