Mbunge adai TRA ni mwiba wa maendeleo ya uchumi

Mbunge wa Viti Maalum (CUF) Riziki Lulida akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Biashara na Viwanda kwa mwaka wa fedha 2019/202 bungeni jijini Dodoma leo.

Muktasari:

  • Mbunge wa Viti Maalum (CUF) Riziki Lulida ameishauri Serikali kuifumua Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa sababu imekuwa mwiba kwa uchumi wa nchi.

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum (CUF) Riziki Lulida amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni mwiba wa uchumi nchini na kutaka ifumuliwe.

Lulida ameyasema hayo bungeni leo Jumanne Mei 14, 2019 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka 2019/2020.

 “Tujipange ukienda Temeke maduka yamefungwa Karikoo yamefungwa matokeo yake wafanyabiashara wanaenda kununua bidhaa Uganda wakati bandari iko hapa,”amesema.

Lulida amesema katika vitu ambavyo vinakwamisha biashara na viwanda nchini cha kwanza ni utendaji wa mamlaka ya mapato nchini.

“TRA ni mwiba wa uchumi wa Tanzania. Watendaji wabovu walioko ndani ya TRA wanafanya nchi hii iyumbe, mimi sitaki kusema ni wapi,”amesema.

Amesema TRA ifumuliwe baada ya Serikali kuangalia mapungufu yako wapi.

Amesema unapotaka kufungua kampuni nchini kabla ya kuanza kazi wanakudai kodi.

“Mwenye kiwanda anavurugu mara Osha, kuna ‘Regulatory Board’ 47 atafanyaje kazi? Tumewakwaza wafanyabiashara matokeo yake tumesimama, mbele hatuendi nyuma hakutikisiki,” amesema.