Mbunge ataka soko la madini Geita, liwe ndilo soko kuu

Muktasari:

Mbunge wa jimbo la Geita Joseph Msukuma amemuomba Waziri Mkuu kuwa soko la madini Geita, liwe soko kuu na wachimbaji wote walitumie hilo badala ya kujenga masoko mengine kila mkoa.

Geita. Wabunge wa mkoa wa Geita wameishukuru Serikali kwa ujenzi wa soko la dhahabu kwa kile walichoeleza kuwa kilikuwa ni kilio cha wachimbaji kwa mrefu, huku wakitaka soko hilo liwe ndilo soko kuu.

Mbunge wa jimbo la Geita Joseph Msukuma akitoa salamu kwa Waziri Mkuu ambaye ni mgeni rasmi wa hafla ya uzinduzi wa soko hilo leo Machi 17, 2019 amemuomba soko hilo, liwe soko kuu na wachimbaji wote walitumie badala ya kujenga masoko mengine kila mkoa

Msukuma amesema uwepo wa soko hilo ni ndoto yake ya tangu mwaka 2013 alipozuia ujenzi wa choo katika eneo lenye soko hilo sasa.

Katika tukio hilo Mbunge wa jimbo la Geita mjini, Constantine Kanyasu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, amesema uamuzi wa madiwani kuridhia jengo hilo kuwa soko la dhahabu utaiwezesha halmashauri kuendelea kuongeza mapato yake.

Mbunge wa jimbo la Busanda, Lorensia Bukwimba amesema pamoja na uwepo wa soko bado wachimbaji wanaomba mazingira rafiki ikiwemo upatikanaji wa umeme wa uhakika.

Mbunge wa Chato ambaye pia ni Waziri wa Nishati na madini, Merdad Kalemani ameomba masoko madogo yafunguliwe katika maeneo mengine ndani ya mkoa huo. Huku akisema umeme unaungwa maeneo yote ya nchi kwa gharama nafuu.