Meneja mawasiliano TFS afariki dunia akizungumza na waandishi wa habari

Muktasari:

Hakuna ajuaye siku wala saa. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya meneja mawasiliano wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Glory Mziray kufariki dunia leo mchana Jumanne Februari 19, 2019


Dar es Salaam. Hakuna ajuaye siku wala saa. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya meneja mawasiliano wa Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Glory Mziray kufariki dunia leo mchana Jumanne Februari 19, 2019.

Glory amefikwa na umauti wakati akizungumza na waandishi wa habari. Hali yake ilibadilika ghafla muda mfupi baada ya kumaliza kusoma taarifa ya TFS kuhusu upandishaji hadhi wa misitu.

Mwananchi lililokuwepo katika kikao hicho lilimshuhudia meneja huyo akizungumza kwa uchangamfu na alipomaliza alionekana kama kuishiwa nguvu na kupoteza fahamu.

Alikimbizwa katika kituo cha Afya TMJ kilichopo Chang’ombe kwa ajili ya matibabu.

Baada ya kumfanyia uchunguzi madaktari wakaeleza kuwa Glory amefariki dunia kabla ya kufikishwa hospitalini hapo.

Upandishaji hadhi misitu

Taarifa aliyoisoma kuhusu kupandishwa hadhi kwa misitu ilieleza kuwa Serikali imeipandisha hadhi misitu saba ambayo ni Itulu, Rondo, Pinndiro, Kalambo, Mwambesi, Aghondi na Kilinga.

Amesema TFS inaendelea na mazungumzo na Serikali za vijiji na zinaridhia kuhifadhi misitu yao ambayo kwa kiwango kikubwa imeharibiwa.

Lengo la jitihada hizo ni kuirudishia misitu hadhi yake ili kufanya uhifadhi kwa faida ya sasa na kizazi kijacho.

Pia aligusia suala la ufugaji nyuki na kuhamasisha wafugaji kufuga kibiashara kwani TFS wanaendelea  kuwatafutia masoko ndani na nje ya nchi.