Meneja mradi wa maji Chato akamatwa kwa agizo la Mbarawa

Muktasari:

  • Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa aagiza meneja wa mradi wa maji wa Imalabupina-Nchankwima kukamatwa kutokana na mradi kuchelewa kukamilika

Chato. Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa ameagiza kukamatwa kwa meneja wa mradi wa maji wa Imalabupina -Nchankwima uliopo wilayani Chato mkoani Geita Bardwin Nzerani hadi atakapokabidhi wizarani nakala za usafirishaji zinazoonyesha muda pampu itakayotolewa nchini Ujerumani kuja Tanzania.

Waziri Mbarawa ametoa agizo hilo leo Ijumaa Aprili 19, 2019 wakati wa ziara yake ya siku moja alipotembelea mradi huo unaojengwa kwa gharama ya Sh8.2 bilioni utakaohudumia vijiji 11 vya wilaya hiyo.

Waziri huyo amesema miradi mingi haikamiliki kutokana na utendaji mbovu wa wakandarasi.

Awali, mkandarasi huyo kutoka kampuni ya Ndeenengo Senguo Co.ltd alisema sababu kubwa ya kuchelewa kwa mradi huo ni kupanuliwa kwa mradi kutoka vijiji viwili hadi 11 na baadhi ya vifaa kusahauliwa hivyo kuwalazimu kurudi kwenye meza kujadiliana.

Amesema sababu nyingine ni kibali cha uagizwaji wa pampu kuchelewa kwa muda wa miezi 18 hadi Machi 26, 2019 ndio walipata kibali na kuagiza pampu kutoka Ujerumani.

Mara baada ya mkandarasi kumalizia kutoa sababu za kuchelewa kwa mradui huo, Waziri Mbarawa alimwagiza Mkuu wa Polisi wa Chato (OCD) kumkamata, agizo ambalo lilitekelezwa mara moja na kumweka kwenye gari la OCD huyo na kuondoka naye.

Awali, Mbunge wa Chato (CCM), Dk Merdad Kalemani amesema changamoto ya mradi huo si fedha bali ni wataalam na kulalamikia mradi kutumia muda mrefu huku wananchi wakiwa na shida ya maji.

Dk Kalemani ambaye pia ni waziri wa nishati, amesema mradi huo ulioanza mwaka 2017 ulipaswa kukamilika Juni 2018 na hadi sasa umekamilika kwa asilimia 80.

Huduma ya maji wilayani Chato inapatikana kwa asilimia 54 huku maeneo mengi ya vijijini yakiwa na changamoto kubwa ya maji safi na salama.