Mgombea DRC akimbilia mahakamani
Muktasari:
- Kanisa Katoliki, lilisema wachunguzi wake 40,000 wa uchaguzi walimpata mshindi tofauti kutoka matokeo rasmi lakini kanisa hilo halikutoa maelezo zaidi
Kinshasa, DRC. Mtihani wa matokeo ya uchaguzi bado unaiandama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) baada ya mshindi wa pili Martin Fayulu kujipanga kuwasilisha pingamizi katika Mahakama ya Katiba.
Mpinzani huyo alisema juzi kwamba atawasilisha pingamizi mahakamani dhidi ya matokeo ya uchaguzi wa Rais yaliyotangaza hivi karibuni.
Muungano wake wa upinzani umesisitiza kwamba, mgombea huyo alipata asilimia 61 ya kura kwa mujibu wa uchunguzi wa waangalizi wa Kanisa Katoliki lenye ushawishi mkubwa .
Fayulu alizungumza na wafuasi wake ambao walikusanyika katika mji mkuu Kinshasa, kupinga kile walichokiita ushindi wa wananchi ulioibiwa.
Fayulu alimtuhumu Rais anayeondoka madarakani Joseph Kabila kwa kufanya makubaliano ya chini kwa chini na mshindi aliyetangazwa, kiongozi wa upinzani Felix Tshisekedi.
Uchunguzi wa Kanisa Katoliki uligundua Tshisekedi alipata asilimia 18 ya kura, juu kidogo ya mgombea wa chama tawala Emmanuel Ramazani Shadary, muungano wa Fayulu ulisisitiza.
Matokeo yachapishwe
Fayulu alitoa wito kwamba Tume ya Uchaguzi (Ceni) ichapishe matokeo, kituo kwa kituo.
"Wale ambao walipanga kuchapisha matokeo bandia, tutapambana nao," alisema Fayulu.
"Nitafanya kila liwezekanalo kwangu kufanya ukweli udhihiri sababu Wacongo wanataka mabadiliko," alisema.
Fayulu hata hivyo ameweka wazi kuwa kuna uwezekano mdogo wa kushinda kesi hiyo kwa sababu mahakama imeundwa na watu wa Kabila lakini alisema hataki kuwapa kisingizio wapinzani wake kuwa hakufuata sheria.
"Tshisekedi ameteuliwa na Kabila ili kutekeleza matakwa ya utawala wa Kabila. Kabila ndiye bosi," alisema Fayulu.
"Kabila hawezi kubaki na kusuka mpango na mtu ambaye hatakuwa na mamlaka yoyote... Tshisekedi anajijua kwamba hakushinda uchaguzi."
Fayulu alisema ana hofu kuwa kutatokea vurumai kama Ceni haitatoa takwimu sahihi za kituo kimoja kimoja cha kupigia kura na kusisitiza kuwa ni haki ya kila Mkongomani kuandamana kwa mujibu wa sheria.
Maelfu ya mashabiki wa Tshisekedi waliingia mitaani kwa furaha kusherehekea ushindi walioupata, lakini upande wa pili wafuasi wa Fayulu walijitokeza kupinga matokeo hayo.
Matukio ya ghasia yaliripotiwa katika eneo la Kikwit, ambapo polisi wawili na raia wawili wanasemakana kuuawa.
Kuna ripoti pia mamia ya wanafunzi wamekuwa wakipinga matokeo hayo kwa kuandamana na kutimuliwa na mabomu ya machozi katika mji wa Mbandaka.
Maandamano pia yameripotiwa katika eneo la Kisangani, lakini Kusini ambapo Tshisekedi anaungwa mkono kwa wingi kumekuwa na sherehe.
Raia wa Congo wanakabiliwa na hali isiyo ya kawaida ya uchaguzi unaodaiwa kuwa umechakachuliwa kuelekea upinzani baada ya mgombea aliyependelewa na Kabila , Shadary , kufanya vibaya katika uchaguzi.
Tume ya Uchaguzi mapema Alhamisi ilitangaza kwamba Tshisekedi alishinda kwa asilimia 38 ya kura wakati Fayulu alipata asilimia 34.
Wakati huohuo vyama vinavyomuunga mkono Rais anayeondoka madarakani nchini humo vimeshinda kwa wingi katika uchaguzi uliocheleweshwa wa Bunge, kwa mujibu wa ukusanyaji wa hesabu uliofanywa na Shirika la Habari la AFP.
Vyama hivyo vimevuka kiwango kwa kupata viti 250 kinachotakiwa kuwa na wingi bungeni katika Bunge la Taifa lenye viti 500, kwa mujibu wa matokeo yaliyowekwa pamoja na Ceni.
Mauaji mji wa Kikwit
Watu watano wanadaiwa kufariki kufuatia maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa rais katika eneo la Magharibi la Kikwit.
Msemaji wa polisi, kanali Pierrot-Rombaut Mwanamputu alithibitisha na kudai kwamba polisi wawili pia walipoteza maisha.
Kwa mujibu wa msemaji huyo wa polisi, mitambo ya kituo cha Radio na Televisheni ya Taifa pia iliharibiwa na waandamanaji hao.