Mhandisi wa Halmashauri atumia nguo zake kujinyonga hadi kufa

Muktasari:

  • Mhandisi wa ujenzi Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya amekutwa kando ya barabara akiwa amejinyonga kwa kujitunduka juu ya mti akitumia nguo zake.

Chunya. Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya jijini Mbeya, Aswile Mssika amekutwa amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kujitunda kwenye mti  akitumia nguo zake katika Kijiji cha kiwanja  wilayani hapa, chanzo cha kuchukua uamuzi huo bado ni kizungumkuti.

Tukio hilo liligundulika juzi Jumatatu mchana ambapo mwili wake ulikutwa kwenye barabara inayokwenda Mlimanjiwa na inadaiwa mtumishi huo alitoweka nyumbani kwake Juni 17 mwaka huu kabla ya kupatikana katika Kijiji hicho.

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Maryprisca Mahundi  licha ya kuthibitisha kutokea kwa taarifa za kifo  cha mtumishi huyo na kutojulikana kwa uwazi juu ya sababu za kujinyonga lakini anahisi huenda ikawa ni tuhuma zilizokuwa zinamkabili kwa vile alikuwa akihojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani hapo kwa kuhusiana na usimamizi wa miradi aliyokuwa akiisimamia.

Amesema mtumishi huyo ambaye alikuwa Mhandisi wa Wilaya Mara ya mwisho kuonana naye ilikuwa Mei 24,2019 ambapo alikuwa amewaita ofisini kwake akiwa na watendaji wenzake na kuwapa maelekezo juu ya usimamizi wa miradi mbalimbali ambayo inaendelea kujengwa  kutokana na kuoneka na dosari ili iweze kurekebishwa.

"Miongoni mwa miradi hiyo ni bwalo la Shule ya Sekondari ya Lupa, nyumba ya walimu ya Chalangwa, madarasa matano Shule ya Sekondari Makalla iliyopo Matundasi na madarasa yanayoendelea kujengwa katika shule ya sekondari Bitmanyanga hii ndio miradi ambayo alikuwa akisimamia kama Mhandisi wa Wilaya, alisema Mahundi.

Mahundi alisema yeye na kamati yake ya ulinzi na usalama baada ya kupata taarifa za kifo hicho waliendelea kufanya uchunguzi na kamati yake iligundua siku mbili kabla ya kifo chake alionekana kama ni mtu mwenye mawazo na alikuwa akinywa zaidi pombe mpaka alipotoweka nyumbani kwake.

Kamanda wa Takukuru wilaya ya Chunya, Lutufyo Mwambungu hakuwa tayari kuzungumzia tukio hilo licha ya kuwepo kwa taarifa kwamba walikuwa wakiendelea kumhoji mtumishi huyo  kwa takribani wiki mbili nyuma.